Marekani yathibitisha kumkamata Rais Maduro wa Venezuela
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135064-marekani_yathibitisha_kumkamata_rais_maduro_wa_venezuela
Rais Donald Trump wa Marekani amethibitisha kuwa nchi yake imemkamata mwenzake wa Venezuela Nicolas Maduro.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 03, 2026 07:29 UTC
  • Marekani yathibitisha kumkamata Rais Maduro wa Venezuela
    Marekani yathibitisha kumkamata Rais Maduro wa Venezuela

Rais Donald Trump wa Marekani amethibitisha kuwa nchi yake imemkamata mwenzake wa Venezuela Nicolas Maduro.

Tangazo la Marekani limejiri baada ya kuripotiwa mashambulio mazito katika mji mkuu wa Venezuela mapema leo Jumamosi.

"Marekani imefanikiwa kutekeleza shambulio kubwa dhidi ya Venezuela na kiongozi wake, Rais Nicolas Maduro, na mke wake wamekamatwa na kuondolewa nchini mwao” Rais Trump ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Christopher Landau, ameandika kwenye jukwaa la X siku ya Jumamosi ya tarehe 3 Januari kwamba Venezuela imepata "mapambazuko mapya" na mtawala wa kiimla hayupo tena na hatimaye atakabiliwa na mkono wa sheria kutokana na makosa yake.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imelaani kitendo cha Marekani cha uchokozi wa kutumia silaha dhidi ya Venezuela na imeelezea wasiwasi wake mkubwa.

Makamu wa Rais wa Venezuela, Delcy Rodríguez, amesema serikali yake haijui mahali alipo Rais Nicolás Maduro wala mkewe, Cilia Flores, kufuatia madai ya Marekani kwamba wamekamatwa baada ya mashambulizi makubwa ya kijeshi.

Akizungumza kupitia televisheni ya taifa, Rodríguez alidai kuwa Marekani inapaswa kutoa “uthibitisho wa uhai” wa Rais Maduro na mke wa rais, akisema serikali ya Venezuela ina wasiwasi mkubwa kuhusu hatima yao

“Tunaitaka serikali ya Marekani kutoa uthibitisho wa uhai wa Rais Maduro na Mama wa Taifa. Rais alikuwa tayari ametuonya kuwa hali kama hii inaweza kutokea,” amenukuliwa akisema, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Venezuela.