Polisi yatumia mabomu ya machozi kudhibiti maandamano Kenya
-
Maandamano ya kumbukuumbu ya miaka miwili ya maandamano ya Gen Z nchini Kenya
Polisi nchini Kenya jana walitumia mabomu ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji katika maeneo mbalimbali mjini Nairobi huku makundi yanayoongozwa na vijana yakifanya kumbukumbu ya miaka miwili tangu maandamano ya Gen Z.
Mawingu mazito ya moshi yalitanda angani huku umati wa watu ukikimbia huku na kule kujinusuru, wengi wao wakifunika nyuso zao kutokana na harufu kali na madhara ya gesi hiyo.
Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi dhidi ya makumi ya vijana na wanaharakati waliokuwa wakitaka kuelekea katika majengo ya bunge la Taifa kuweka shada za maua kuwakumbuka vijana waliouawa miaka miwili iliyopita. Vijana hao walilazimika kutawanyika kuelekea mzunguko mkubwa wa Globe.
Makabiliano kama hayo yalizuka karibu na Chuo Kikuu cha Nairobi na kando ya Barabara ya University Way, ambapo wanafunzi na waandamanaji wengine walikabiliana na polisi wa kutuliza ghasia waliokuwa wakijaribu kuwazuia kuingia CBD.
Viongozi wa Upinzani, wanaharakati na ndugu wa waathiriwa hawakuruhusiwa kuweka mashada ya maua kwenye bunge ambapo tukio la mauaji lilitokea kwani eneo hilo lililikuwa limezingirwa na nyaya huku polisi wakiweka ulinzi mkali.
Matukio haya yanajiri wakati Wakenya wanakumbuka maandamano ya Juni 25, 2024 dhidi ya Mswada tata wa Fedha, yaliyogeuka kuwa machafuko ya kitaifa na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 120 kulingana na mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Maandamano ya jana kwa kiasi kikubwa yalielezwa kuwa ya amani, yakilenga kuwakumbuka waliopoteza maisha huku yakitaka haki, uwajibikaji kwa vitendo vya ukatili vinavyodaiwa kufanywa na polisi, pamoja na kukomeshwa visa vya utekaji nyara na mauaji ya kiholela.