Muqawama: Mashambulizi ya Venezuela yameanika dhati ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i135108-muqawama_mashambulizi_ya_venezuela_yameanika_dhati_ya_marekani
Makundi ya Muqawama katika eneo la Asia Magharibi sanjari na kulaani kile yalichokiita ugaidi wa kiserikali wa Marekani dhidi ya Venezuela, yamesema mashambulizi na utekaji nyara wa Rais Nicolas Maduro wa Venezuela kwa mara nyingine tena umeanika dhati na hulka halisi ya Marekani.
(last modified 2026-01-04T08:42:17+00:00 )
Jan 04, 2026 08:42 UTC
  • Muqawama: Mashambulizi ya Venezuela yameanika dhati ya Marekani

Makundi ya Muqawama katika eneo la Asia Magharibi sanjari na kulaani kile yalichokiita ugaidi wa kiserikali wa Marekani dhidi ya Venezuela, yamesema mashambulizi na utekaji nyara wa Rais Nicolas Maduro wa Venezuela kwa mara nyingine tena umeanika dhati na hulka halisi ya Marekani.

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imelaani vikali uchokozi wa Marekani dhidi ya Venezuela na kutekwa nyara kwa Rais Nicolás Maduro, na kuelezea hatua hiyo kama "ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa" na "hujuma dhidi ya mamlaka ya nchi huru."

"Uchokozi huu unaashiria muendelezo wa sera zisizo za haki za Marekani na uingiliaji kati, ambao unasukumwa na matarajio yake ya kibeberu," kundi hilo lenye makao yake makuu huko Gaza limesema katika taarifa yake ya jana Jumamosi.

Hamas imeongeza kuwa, sera hizo za Marekani "zimeyaingiza mataifa kadhaa katika msukosuko, na ni tishio la moja kwa moja kwa amani na usalama wa kimataifa."

Nayo Harakati Jihadul Islami ya Palestina pia imesema mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela yamefichua dhati ya wazi ya ubeberu, uvamizi na utumiaji mabavu wa Marekani.

Harakati ya Muqawama imesema katika taarifa kwamba, shambulio hilo lilikuwa ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na uhuru wa kitaifa, na lilionyesha mkakati mpana wa ubeberu, wa kudhibiti mataifa na kupora mali zao. Kundi hilo la Muqawama limetangaza mshikamano kamili na Venezuela, raia wake na serikali yao halali inayoongozwa na Rais Nicolas Maduro.

Kwa upande wake, afisa wa ngazi ya juu wa Harakati ya Muqawama ya Ansarullah ya Yemen amesema hulka halisi ya serikali ya Marekani imezidi kudhihirika baada ya Rais Donald Trump kutangaza kuwa Marekani imefanya "shambulio kubwa la kijeshi" dhidi ya Venezuela na kumteka nyara Rais Nicolas Maduro. Nasruddin Amer, Naibu Mkurugenzi wa ofisi ya vyombo vya habari ya vuguvugu hilo, alisema hayo katika chapisho lililochapishwa kwenye kanali yake ya Telegram Jumamosi usiku.