Wanajeshi wengine 4 wa Israel waangamizwa katika mashambulizi tofauti Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128334
Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti habari ya kuangamizwa wanajeshi wanne wa Kizayuni katika mashambulizi tofauti katika Ukanda wa Gaza jana Jumatatu.
(last modified 2025-07-19T08:58:23+00:00 )
Jul 14, 2025 16:00 UTC
  • Wanajeshi wengine 4 wa Israel waangamizwa katika mashambulizi tofauti Gaza

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti habari ya kuangamizwa wanajeshi wanne wa Kizayuni katika mashambulizi tofauti katika Ukanda wa Gaza jana Jumatatu.

Kwa mujibu wa ripoti hizo, mashambulizi hayo yalitokea katika maeneo tofauti ya Gaza, ikiwa ni pamoja na Khan Younis, Jabalia, kitongoji cha Al-Tuffah, na Al-Shuja'iyya.

Hapo awali, tovuti ya Palestine Online iliripoti kwamba, takriban wanajeshi wawili wa Israel waliuawa na wengine wawili kujeruhiwa wakati wanamapambano wa Kipalestina walipolenga gari la kijeshi kwa roketi.

Vyanzo vya habari vya Israel baadaye vilithibitisha kuwa mashambulizi manne tofauti yalifanyika, na hivyo kuongeza idadi ya waliouawa kufikia wanne.

Vyombo vya habari vya Israel vimemlaani Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu kwa kutuma wanajeshi wa utawala huo kufa katika "vita visivyo na maana" ili tu kulibakisha baraza lake la mawaziri madarakani.

Haya yanajiri siku chache baada ya wanamapambano wa Harakati ya Hamas kufanya shambulizi la kuvizia la awamu nne huko Beit Hanoun na kuua wanajeshi watano wa Israel na kuwajeruhi wengine 14.

Licha ya mauaji ya kimbari yanayoendelea dhidi ya watu wa Gaza kwa zaidi ya miezi 21 sasa, lakini utawala wa Kizayuni umeshindwa kuvunja irada na azma ya wananchi na wanamuqawama wa Hamas.