Hamas yataka kukomeshwa sera ya Israel ya kuwaua Wapalestina kwa njaa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128612-hamas_yataka_kukomeshwa_sera_ya_israel_ya_kuwaua_wapalestina_kwa_njaa
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imekaribisha taarifa ya pamoja ya Uingereza na nchi nyingine 24, zikitaka kusitishwa mara moja vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza na kuingizwa haraka misaada ya kibinadamu katika ukanda huo uliozongirwa.
(last modified 2025-10-20T07:03:11+00:00 )
Jul 22, 2025 05:08 UTC
  • Hamas yataka kukomeshwa sera ya Israel ya kuwaua Wapalestina kwa njaa

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imekaribisha taarifa ya pamoja ya Uingereza na nchi nyingine 24, zikitaka kusitishwa mara moja vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza na kuingizwa haraka misaada ya kibinadamu katika ukanda huo uliozongirwa.

Waitifaki wa Israel, yaani Uingereza, Ufaransa, Australia, Canada na nchi nyingine 21, pamoja na Umoja wa Ulaya, zilisema katika taarifa ya pamoja jana Jumatatu kwamba, mateso katika Ukanda wa Gaza "yamefikia kina kipya" na kwamba vita "lazima vikome sasa."

Katika taarifa hiyo, nchi hizo zimelaani "kuingizwa misaada (Gaza) kwa njia ya matone, na mauaji ya kinyama ya raia, wakiwemo watoto wanaotaka kukidhi mahitaji yao ya kimsingi ya maji na chakula."

Hamas imesema taarifa hiyo ya pamoja ya kutambua sera ya njaa ya Israel kama ukiukaji wa wazi wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu inaashiria hatua muhimu kuelekea uwajibikaji wa kimataifa.

"Kitendo cha utawala wa Israel kuzuia msaada muhimu wa kibinadamu kuwafikia raia hakikubaliki. Israel lazima itii wajibu wake chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu." Hamas imesema katika taarifa yake.

Harakati hiyo ya Muqawama imepongeza tamko hilo la kulaani mauaji ya zaidi ya raia 800 wa Kipalestina katika vituo vya kusambaza misaada vya Marekani na Israel, ambayo imesema "yanathibitisha ukatili wa utaratibu huu, malengo yake ya jinai ya kuua na kuwadhalilisha watu wetu, haja ya haraka ya kusambaratisha na kuwawajibisha waendeshaji wake."