Hamas: Israel lazima igharamie ujenzi mpya wa Gaza
Afisa mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, Mousa Abu Marzouk ametoa wito kwa Israel kufadhili kikamilifu ukarabati na ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza, akitaja uharibifu mkubwa na haki za Wapalestina zaidi ya milioni mbili ambao wamepoteza makazi yao, makazi na riziki.
Abu Marzouk amebainisha kuwa, "Kuijenga upya Gaza ni haki kwa watu wa Palestina. Wakaliaji ardhi kwa mabavu (Israel) wana wajibu wa kubeba gharama kamili. Ujenzi mpya lazima uwe wa haraka, wa kina, na ujumuishe miundombinu, huduma za afya, barabara, mitambo ya umeme na mifumo ya maji."
Makadirio ya kimataifa yanaweka gharama ya kuijenga upya Gaza kati ya dola bilioni 50 na bilioni 80. Zaidi ya 70% ya uharibifu umejikita katika sekta ya makazi, na kuwalazimisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao.
Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linasisitiza kuhusu udharura wa kujengwa upya Gaza na kuiwajibisha Israel kwa uharibifu huo.
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amesisitiza kuwa, "Israel lazima igharamie ujenzi mpya wa Gaza."
Kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Serikali katika Ukanda wa Gaza, asilimia 90 ya miundombinu ya Gaza imeharibiwa kabisa baada ya vita vya miaka miwili vilivyoanzishwa na utawala ghasibu wa Israel.
Aidha ripoti rasmi zikieleza kuwa, mashambulizi ya utawala ghasibu wa Israel yameharibu asilimia 97 ya shule za Ukanda wa Gaza na hivyo kuhatarisha mustakbali wa kielimu wa wanafunzi laki tatu wa Kipalestina katika eneo hilo.