Trump: Ukraine haiwezi kushinda vita dhidi ya Russia
Rais wa Marekani, Donald Trump amesema haitakidi kwamba Ukraine inaweza kuibuka mshinda katika vita vyake na Russia.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House jana Jumatatu, Trump alisema "Bado wanaweza kushinda. Sidhani wataishinda, lakini bado wanaweza kushinda," alipoulizwa kufafanua msimamo wake kuhusu mzozo huo.
"Nilisema wanaweza kushinda. Lolote linaweza kutokea. Unajua, vita ni jambo la ajabu sana. Mambo mengi mabaya hutokea. Mambo mengi mazuri hutokea," alisema.
Alipoulizwa kuhusu madai ya shambulio la Russia katika maeneo ya raia nchini Ukraine, alijibu kwamba wengi wa waliouawa walikuwa wanajeshi. Trump pia amedai kuwa karibu wanajeshi 5,000 hadi 7,000 wa pande zote mbili huuawa kila wiki katika mzozo huo.
Aidha itakumbukwa kuwa, Trump mwenyewe alidai mwezi uliopita kwamba Ukraine inaweza kushinda kijeshi na kuteka tena maeneo yote yanayokaliwa na Russia, ambayo yanajumuisha pia Rasi ya Crimea na maeneo mengine ya mashariki mwa Ukraine.
Rais wa Marekani, ambaye aliahidi kuvimaliza haraka vita kati ya Russia na Ukraine, anatazamiwa kukutana na mwenzake wa Russia Vladimir Putin, nchini Hungary mnamo wiki zijazo.
Trump ametoa wito kwa Russia na Ukraine kusimamisha vita katika mstari wa mapigano zilipo hivi sasa, pendekezo ambalo litaiwezesha Moscow kuhodhi sehemu kubwa ya maeneo ya ardhi ya Ukraine.