Baadhi ya Waislamu waanza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i136758-baadhi_ya_waislamu_waanza_funga_ya_mwezi_mtukufu_wa_ramadhani
Baadhi ya nchi za Waislamu na Kiarabu zimetangaza leo Jumatano kuwa siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
(last modified 2026-02-18T07:37:01+00:00 )
Feb 18, 2026 06:24 UTC
  • Baadhi ya Waislamu waanza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani

Baadhi ya nchi za Waislamu na Kiarabu zimetangaza leo Jumatano kuwa siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Tovuti ya habari ya Mehr imenukuu Al Jazeera ikiripoti kuwa, baadhi ya nchi za Kiarabu zimetangaza leo Jumatano, kuwa siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Nchi kama vile Saudi Arabia, Qatar, Kuwait, Umoja wa Falme za Kiarabu, Yemen, Palestina na Lebanon zimeanza kutekeleza faradhi hiyo na nguzo ya nne ya Uislamu leo.

Nchi zingine kama vile Oman, Jordan, Syria na Misri zimetangaza kwamba kesho Alkhamisi ndiyo mwanzo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kadhalika Waislamu katika nchi za Afrika wamegawanyika, ambapo kuna wale walioanza funga ya Ramadhani leo huku wengine wakitazamiwa kuanza kesho, kwa kuwa mwezi haukuandama hiyo jana katika nchi zao.

Ramadhani ni mwezi wa 9 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria, mwezi wa baraka na ibada ambao ndani yake kiliteremshwa kitabu kitukufu cha Qur'ani.

Idhaa ya Kiswahilii ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawatakia Waislamu wote ulimwenguni Ramadhani Mubarak na funga njema pamoja na kutakabaliwa Saumu na ibada zao katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.