Alkhamisi, 19 Februari, 2026
Leo ni Alkhamisi tarehe Mosi Ramadhani 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe 19 Februari, 2026.
Leo ni siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria; mwezi ambao ndani yake iliteremshwa Qur'ani Tukufu.
Ni mwezi wa rehema na baraka tele. Katika kubainisha utukufu wa mwezi huu, Mtume Muhammad (saw) amesema, siku za mwezi huu ndizo siku bora zaidi kuliko siku nyingine zote na amewataka Waislamu wachume na wafaidike kutokana na fadhila na baraka za kiroho za mwezi huu. Allah SW anasema katika kitabu chake kitukufu kwamba: (Hakika tumeiteremsha Qur'ani katika usiku wa heshima. Na nini kitakujulisha usiku huo wa heshima ni nini? Laylatul Qadr (usiku huo wa heshima) ni bora kuliko miezi elfu.)
Tukio la kuhuzinisha moyo la kuuawa shahidi Imam Ali bin Abi Twalib (as) na lile la kuzaliwa mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hassan (as), ni katika matukio muhimu yaliyotimia katika mwezi huu. Tunamuomba Allah SW atupe baraka za Ramadhani, na kwa fadhila za mwezi huu mtukufu tuwe karibu na rehema na msahamaha Wake. ***
Katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, kiliteremshwa kitabu cha Suhuf cha Nabii Ibrahim (as).
Jina Ibrahim limetajwa mara 69 katika Qur'ani Tukufu kwa heshima na taadhima ambapo maisha yake yameashiriwa kwa njia mbalimbali kama ibra na ruwaza njema kwa waumini. Mwenyezi Mungu SW amemtaja kuwa ni mtu mwenye kumuabudu Mungu Mmoja, na dini yake imetajwa kuwa ya Hanif katika Aya ya 67 ya Suratu Aal Imran na pia katika Aya ya 125 ya Suratu An Nisaa.
Alikuwa Nabii mkweli kama tunavyosoma katika Suratu Maryam Aya ya 41. Aidha Mwenyezi Mungu alimpa yeye na familia yake neema na mamlaka kama tunavyosoma katika Suratu Nisaa Aya ya 54.
Kuna vitabu kadhaa vya mbinguni ambavyo waliteremshwa kwa Mitume wa Mungu kama vile Suhuf vya Ibrahim na Nuh (AS), Taurati ya Musa (AS) na Injili ya Isa (AS), na kitabu kilicho kamilika kati ya vyote ni Qur'ani Tukufu. ****
Katika siku kama ya leo miaka 1019 iliyopita alifariki dunia Ibn Sina maarufu kwa jina la Sheikhur Rais, tabibu, mtaalamu wa hisabati, falsafa na mnajimu mkubwa wa Kiirani.
Ibn Sina alifariki dunia katika mji wa Hamadan ulioko magharibi mwa Iran akiwa na umri wa miaka 58. Alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana na akapata kusoma elimu za mantiki, uhandisi na utaalamu wa nyota. Baada ya kumtibu Nuh bin Mansur, mmoja wa Wafalme wa Kisamani akiwa kijana, Ibn Sina alipata idhini ya kutumia maktaba kubwa ya mfalme huyo. Katika maktaba hiyo, Ibn Sina alipata kusoma vitabu vingi vya elimu tofauti. Abu Ali Sina alitokea kuwa msomi, mwandishi na mtafiti mashuhuri.
Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha "Shifaa" kinachohusu elimu ya falsafa, "Qanun" kinachohusu tiba na "Daneshnameh Allai". *****
Katika siku kama ya leo miaka 715 iliyopita, alizaliwa Ibn Khaldun, mtaalamu wa masuala ya kijamii, mwanasiasa na mwanahistoria Mwislamu.
Ibn Khaldun alizaliwa huko Tunisia. Maisha ya Ibn Khaldun yanaweza kugawanywa katika sehemu tatu na sehemu ya kwanza aliitumia katika kusoma elimu tofauti. Alitumia sehemu ya pili ya maisha yake katika siasa na kuhudumia nyadhifa tofauti za utendaji na alifungwa jela kutokana na njama za maadui zake.
Baada ya kuachiliwa huru Ibn Khaldun alijitenga na siasa. Hapo ndipo ilipoanza duru ya tatu ya maisha yake ambapo alijishughulisha na utafiti na uandishi. Alimu na msomi huyo alifariki dunia mwaka 808 Hijiria.
Miongoni mwa kazi muhimu za Ibn Khaldun, tunaweza kutaja kitabu chake maarufu kuhusu historia. Jina la kitabu hiki linaanza na neno "Al-Ebar" (somo) na kinajulikana kama "Tarikh Ibn Khaldun". Kitabu hiki kina juzuu saba na kina utangulizi mrefuu unaojulikana kama "Muqaddimatu Ibn Khaldun." Alifariki dunia mwaka wa 808 Hijria. ******
Siku kama ya leo miaka 553 iliyopita alizaliwa mnajimu na mwanahesabati mashuhuri wa Poland, Nicolaus Copernicus.
Awali alijifunza elimu ya nujumu na baadaye tiba, na baada ya kukamilisha masomo alianza kufundisha hesabati huko Roma. Hata hivyo Copernicus aliendelea kudurusu na kufanya utafiti wa elimu ya nujumu na mwaka 1503 alivumbua nadharia ya harakati ya dunia kuzunguka jua na vilevile dunia kujizunguka yenyewe katika kila baada ya masaa 24.
Nicolaus Copernicus alifariki dunia tarehe 24 Mei 1543 siku chache tu baada ya kuchapisha kitabu cha On the Revolutions of the Celestial Spheres kinachofafanua nadharia zake. ***
Miaka 75 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 19 Februari mwaka 1951 alifariki dunia mwandishi na mkosoaji mashuhuri wa Ufaransa, Andre Gide, akiwa na umri wa miaka 82.
Alizaliwa mwaka 1869 Miladia mjini Paris lakini alitumia umri wake mwingi Afrika kaskazini na hasa nchini Algeria. Visa vingi alivyoandika viliathiriwa na maisha pamoja na utamaduni wa watu bara hilo. Miongozi mwa visa vya kuvutia vilivyoandikwa na mwandishi huyo ni pamoja na "Wimbo wa kijijini" na "Meza ya Ardhi." Mwaka 1947 Gide alitunukiwa zawadi ya Nobel. ***
Miaka 74 iliyopita katika siku kama ya leo mwaka 1952 alifariki dunia mwandishi wa Norway, Knut Hamsun. Alizaliwa mwaka 1859 katika familia masikini kaskazini mwa nchi hiyo, na alipotimiza miaka 24 aliingia katika uwanja wa uandishi.
Hamsun alisafiri mara mbili kwenda Marekani na akaandika makosa aliyoyaona nchini humo ndani ya kitabu alichokipa anwani ya "Maisha ya Kimaanawi katika Zama Mpya Nchini Marekani" pia aliandika kitabu kilichopewa jina la "Njaa" ambacho kilibeba tamaduni mbali mbali za dunia.
Uandishi wake wa kitabu cha "Matunda ya Ardhini" ulikuwa na nafasi muhimu katika kutunukiwa zawazi ya Nobel mwaka 1920. ****
Tarehe 19 Februari miaka 29 iliyopita alifariki dunia Deng Xiaoping, kiongozi wa zamani wa China na mhandisi wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ya nchi hiyo.
Katika kipindi cha uongozi wa Xiaoping China ilifanya mageuzi makubwa katika nyanja mbalimbali na alifanya marekebisho makubwa katika uchumi wa kisoshalisti wa wakati huo wa China na kuuelekeza kwenye uchumi wa soko. Wakati huo China ilifanikiwa kuingia katika nyanja mbalimbali za kimataifa na kutatua migogoro iliyokuwepo katika uhusiano wake na nchi kadhaa.
Deng Xiaoping alijiuzulu mwaka 1990 kutokana na maradhi na umri wake mkubwa na hadi anafariki dunia alikuwa akihesabiwa kuwa shakhsia mkubwa zaidi wa China. ***
Miaka 16 iliopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 30 Bahman 1388 Hijiria Shamsia, manowari ya kwanza ya kivita ya Iran inayojulikana kwa jina la Jamaran ilianza kufanya kazi.
Jamaran ni manowari ya kijeshi yenye uwezo wa kubeba aina kadhaa za makombora ya kuhujumu meli na kutungua makombora na ndege za adui. Pia ina rada za kisasa na uwezo wa kushiriki katika vita vya kielektroniki.
Meli hiyo inayoenda kwa kasi kubwa pia ina eneo la kutua helikopta. Baadhi ya teknolojia iliyotumia kutengeneza manuwari hiyo inamilikiwa na nchi kadhaa tu dunia na wataalamu wa Jamhuri ya Kiislamu wamefanikia kuvunja mzingiro huo na kuiwezesha Iran kuwa miongoni mwa nchi zenye utaalamu wa kubuni na kuzalisha teknolojia hiyo. ***