Namna Nguvu Dhaniwa ya Ulaya Ilivyosambaratika?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140272-namna_nguvu_dhaniwa_ya_ulaya_ilivyosambaratika
Esmaeil Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, huku akijibu karibuni hivi hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuiwekea Iran vikwazo vipya kwa kisingizio cha kutetea haki za binadamu, amesema: "Madai ya Umoja wa Ulaya kuhusu kutetea haki za binadamu za wananchi wa Iran ni unafiki mtupu."
(last modified 2026-07-30T04:44:29+00:00 )
Jul 30, 2026 04:34 UTC
  • Namna Nguvu Dhaniwa ya Ulaya Ilivyosambaratika?

Esmaeil Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, huku akijibu karibuni hivi hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuiwekea Iran vikwazo vipya kwa kisingizio cha kutetea haki za binadamu, amesema: "Madai ya Umoja wa Ulaya kuhusu kutetea haki za binadamu za wananchi wa Iran ni unafiki mtupu."

Akiandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa Kaja Kallas, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, anazungumzia "hoja za umoja huo kuhusu haki za binadamu" nchini Iran; katika hali ambayo inashangaza kuona namna kanuni hii ya eti kutetea haki za binadamu inavyotoa msaada wa kiufundi na kimkakati kwa ajili ya kufanyika mashambulizi haramu ya kijeshi dhidi ya wananchi wa Iran na miundombinu ya taifa hili, huku ikikwepa kulaani jinai za wazi dhidi ya binadamu au hata kutoa rambirambi za kawaida kwa familia za watoto wa Iran waliouawa kinyama na kupata ulemavu katika mashambulizi hayo. Ameongeza: "Tabia hii haiondoi tu itibari bali ni kilele cha uovu na unafiki."

Ingawa matamshi haya yametolewa katika kujibu vikwazo vipya vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran, lakini ni ishara ya malalamiko kuhusu mgogoro mkubwa zaidi ambao unatilia shaka madai ya nchi za Magharibi kuhusu suala zima la haki za binadamu. Suala hili si mzozo kati ya Iran na Ulaya pekee, bali ni suala la msingi linalohusu ulimwengu mzima. Inasikitisha kuona kuwa jambo hili limebadilishwa kuwa chombo cha kuwashinikiza wapinzani, huku likifumbia macho mateso yanayofanywa dhidi ya wahanga na waathirika walio upande mwingine wa milinganyo ya kijiopolitiki.

Vikwazo vilivyowekwa karibuni dhidi ya majaji kadhaa wa Iran kwa kisingizio cha "kukiuka haki za binadamu" vimetangazwa wakati ambao maoni ya umma kimataifa yalikuwa yanasubiri kupata jibu la wazi kuhusu moja ya maafa ya kibinadamu ya kusikitisha zaidi kuhusiana na vita vya kichokozi vya hivi karibuni vya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran, shambulio dhidi ya Shule ya "Shajareh-ye Tayyebeh" mjini Minab. Mnamo tarehe 28 Februari, siku ya kwanza ya uchokozi wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, shule ya Shajareh-ye Tayyebeh iliyoko katika mji wa Minab, kusini mwa Iran, ni miongoni mwa maeneo yaliyolengwa kwa makombora ya Marekani aina ya Tomahawk. Katika shambulio hilo, watoto 168 walipoteza maisha ambapo kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, miili yao ilikatwakatwa vipande vipande. Miezi mitano baadaye, mabaki ya miili ya baadhi ya watoto hao yalipatikana na kutambuliwa, ingawa hakuna athari yoyote iliyopatikana kuhusiana na watoto wawili kati yao. Uchunguzi wa ndani wa jeshi la Marekani unaonyesha kuwa shambulio hilo, ambalo lilifanywa kwa makusudi kupitia mashambulio mawili tofauti ya makombora dhidi ya shule hiyo ya msingi, lilikiuka viwango vyote vya haki za binadamu na sheria za kimataifa. Umoja wa Mataifa pia umeanzisha uchunguzi huru kuhusiana na shambulio hilo. Swali linalojitokeza hapa ni kuwa je, ni wapi katika taarifa za Umoja wa Ulaya tunaweza kuona ishara ya hasira ya kimaadili inayodaiwa na umoja huo kuhusiana na suala zima la haki za binadamu wakati unapoweka vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran? Ni afisa yupi wa Ulaya aliyewahi kutoa wito wa kuwekewa vikwazo wale waliohusika na jinai hii ya Minab? Ni taasisi gani ya Ulaya imewahi kushinikiza kuundwa kwa kamati huru ya kutafuta ukweli kwa mkazo na sisitizo lile lile linalotumika kuhusu matukio mengine kama hayo? Kama wahanga wa shambulio hili wangekuwa watoto wa nchi za Ulaya, je, wito wa Brussels ungeishia tu kwenye maneno machache ya kuelezea wasiwasi? Itibari ya mfumo wowote wa haki za binadamu haipimwi kwa idadi ya taarifa zinazotolewa, bali kwa uthabiti wa viwango vyake. Ikiwa haki za binadamu zinapaswa kuheshimiwa kwa usawa kimataifa, hazipaswi kupimwa kwa viwango tofauti vya pasipoti za waathirika, bendera za nchi wala utambulisho wa wahusika wa jinai zinazotekelezwa. Thamani ya maisha ya mtoto wa Minab haipaswi kuwa ndogo kuliko ya mtoto wa mahala pengine popote duniani.

Mgongano mkubwa zaidi hudhihiri hadharani pale Ulaya inapodai kuwa inatetea mfumo unaozingatia kanuni na sheria, lakini, wakati washirika wake wanapohusika katika jinai dhidi ya binadamu hupindisha kirahisi sheria hizo hizo na bila kujali lolote kwa shabaha ya kuwalinda wahalifu. Kwa watu wengi wenye mawazo huru na watetezi wa uhuru duniani, tabia hii si kutetea haki za binadamu, bali ni "uteuzi wa kisiasa wa wahanga", jambo ambalo kabla ya suala jingine lolote hudhoofisha pakubwa imani ya dunia kwa taasisi za haki za binadamu. Matukio ya hivi karibuni yameongeza mgawanyiko na tofauti zilizopo kuhusu suala hili; hata ndani ya Marekani kwenye, ambapo sasa vyombo vya habari, wabunge na mashirika ya haki za binadamu yanataka kuwekwa wazi matokeo ya uchunguzi wa Pentagon kuhusu shambulio la Minab na wakati huo huo kukosoa usiri mkubwa unaofanyika kuhusiana na suala hili. Leo hii, Ulaya inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kutoaminika kuliko makabiliano yake na Iran. Hata kama kuiwekea Iran vikwazo kunaweza kuigharimu Tehran kisiasa, lakini hatua hiyo haiwezi kuondoa swali la msingi kuhusu sababu zinazofanya haki za binadamu ndani ya mfumo wa sera za kigeni za Brussels, kuyumbayumba kati ya kuwa kanuni isiyoweza kubadilika na maana inayobadilikabadilika kimaslahi kila siku kuhusu suala hilo. Jibu la Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, kuhusiana na undumakuwili wa kuaibisha wa Ulaya katika kuiwekea Iran vikwazo vipya kwa kisingizio cha haki za binadamu, linaakisi mgogoro ambao umekuwepo kwa muda mrefu katika kiini cha sera za kigeni za Ulaya, mgogoro ambao unazidi kuongezeka kila siku kutokana vipimo viwili tofauti kati ya madai ya "madai ya kimaadili" na "mwenendo halisi wa kisiasa". Madamu Umoja wa Ulaya hautaziba pengo hili, vikwazo vyovyote vipya dhidi ya Iran, kabla ya kupata uhalali wowote wa kisheria vitaendelea kuibua maswali mapya kuhusu uhalali wa kimaadili wa umoja huo wenyewe kuhusiana na suala zima la haki za binadamu.