Waziri wa zamani Kenya: Rais Ruto anawalazimisha mawaziri kufanya anachotaka kwa woga
-
Prof Njuguna Ndung’u
Waziri wa zamani wa Fedha wa Kenya, Prof Njuguna Ndung’u, amemshutumu Rais wa nchi hiyo, William Ruto kwa kuingilia utendakazi wa taasisi huru, akisema mtindo huu umezorotesha uwezo wa kutekeleza majukumu ipasavyo.
Akizungumza katika mkutano kuhusu misaada nchini Uswizi, Prof Ndung’u amesema taasisi nyingi zina uwezo wa kufanya maamuzi sahihi lakini zinalemazwa na kile alichokitaja kuwa ni tabia ya mtu mmoja kutaka kudhibiti kila kitu.
"Rais wa sasa wa Kenya anaingilia utendakazi wa taasisi zote", amesema Prof Ndung’u, na uiongeza kuwa maafisa wengi wa serikali hulazimika kufuata maagizo kwa hofu.
Amesema, akiwa Waziri wa Fedha alikataa kushiriki mikataba au mipango ambayo haikuwa sahihi.
Hii ni mara ya kwanza Prof Ndung’u kuzungumzia hadharani changamoto alizokumbana nazo akiwa katika serikali ya Rais William Ruto kabla ya kuondolewa madarakani katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofuatia maandamano ya Gen Z dhidi ya Muswada wa Fedha wa mwaka 2024.
Matamshi hayo ya waziri wa zamani wa fedha wa Kenya zimeibua tena mjadala kuhusu mtindo wa uongozi wa Rais Ruto.
Wakosoaji wanasema anapenda kusimamia karibu kila uamuzi wa serikali, huku wafuasi wake wakimtetea wakisema ni kiongozi anayefuatilia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya serikali.
Prof Njuguna Ndung’u pia amekosoa sera ya kuongeza ushuru ili kuimarisha mapato ya serikali, akisema ushuru mkubwa mara nyingi hupunguza mapato badala ya kuyaongeza.