Watu kadhaa wafa maji, mamia ya Wamorocco wakimbilia Ceuta ya Uhispania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140306-watu_kadhaa_wafa_maji_mamia_ya_wamorocco_wakimbilia_ceuta_ya_uhispania
Wimbi la wahamiaji kutoka Morocco kuelekea mji unaodhibitiwa na Uhispania wa Ceuta limegeuka kuwa mgogoro wa kibinadamu na kisiasa, baada ya miili ya wahamiaji tisa kuopolewa majini. Wahamiaji hao waliaga dunia wakiwa katika jitihada za kuogelea hadi mjini huo.
(last modified 2026-07-31T08:41:02+00:00 )
Jul 31, 2026 08:37 UTC
  • Wimbi la wahamiaji kuelekea Uhispania
    Wimbi la wahamiaji kuelekea Uhispania

Wimbi la wahamiaji kutoka Morocco kuelekea mji unaodhibitiwa na Uhispania wa Ceuta limegeuka kuwa mgogoro wa kibinadamu na kisiasa, baada ya miili ya wahamiaji tisa kuopolewa majini. Wahamiaji hao waliaga dunia wakiwa katika jitihada za kuogelea hadi mjini huo.

Ni baada ya serikali ya Uhispania kutangaza kwamba miili ya ya wahamiaji tisa waliokufa maji imeopolewa baharini baada ya kufariki dunia wakijaribu kuelekea katika mji wa Ceuta ulioko kaskazini mwa Morocco kwenye Bahari ya Mediterania.

Haya yanajiri huku kukiwa na wimbi la mamia ya wahamiaji, wengi wao kutoka Morocco, wanaoelekea Ceuta, kufuatia kuwasili wahamiaji zaidi ya 1,500 walioogelea kutoka Morocco katika siku za hivi karibuni, na kuilazimisha serikali ya Uhispania kutuma jeshi katika eneo hilo.

Huu ndio msafara mkubwa zaidi wa wahamiaji kutoka Morocco kuelekea mji wa Ceuta - wengi wao wakiwa wanaume na vijana - tangu mwaka 2021, wakati wahamiaji wapatao 10,000 walipowasili kwenye eneo hilo linalomilikiwa na Uhispania kufuatia mgogoro wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Jana Alkhamisi Serikali ya Uhispania katika mji wa Ceuta ililitaka jeshi la kuingilia kati ili kuzuia wimbi la maelfu ya watu kuvuka mpaka bila vibali.

Kwa kuzingatia wimbi kubwa la wahamiaji, Gavana wa Ceuta, Juan Jesus Vivas amesema katika mahojiano yaliyotangazwa kwenye televisheni ya Uhispania kwamba: "Tunakabiliwa na dharura ya kibinadamu na kijamii."

Mamlaka ya Morocco bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu kadhia hiyo, lakini chanzo rasmi cha Morocco kimeiambia AFP kwa sharti la kutotajwa jina kuwa nchi hizo mbili zimezungumza kuhusu suala hilo.

Uhamaaji wa watu kutoka Morocco hadi maeneo mawili ya Ceuta na Melilla yanayodhibitiwa na Uhispania, kwa muda mrefu umekuwa suala nyeti la kisiasa kati ya nchi hizo mbili.