Algeria na Italia zakubaliana kuimarisha ushirikiano ili kupambana na uhamiaji haramu
-
Algeria na Italia kuimarisha ushirikiano dhidi ya uhamiaji haramu
Algeria na Italia zimekubaliana kuimarisha ushirikiano dhidi ya uhamiaji haramu na uhalifu wa kuvuka mipaka. Uamuzi huu umefikiwa wakati wa mazungumzo kati ya Mawaziri wa Mambo ya Ndani wan chi mbili hizo huko Roma, Italia.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Algeria imeeleza kuwa Said Sayoud Waziri wa Mambo ya Ndani wa Algeria na mwenzake wa Italia, Matteo Piantedosi wamechunguza na kujadili njia za kuimarisha ushirikiano wa pande mbili ili kudhibiti uhamiaji usio wa kawaida na kusambaratisha mitandao ya magendo ya wahamiaji na biashara ya kusafirisha binadamu kinyume cha sheria.
Wizara hiyo imeeleza kuwa upande wa Italia umepongeza juhudi za Algeria katika kupambana na wahamiaji haramu na "mkakati mkubwa wa nchi hiyo unaoshirikisha hatua za kibinadamu, kiusalama na kimaendeleo ili kushughulikia changamoto za uhamiaji barani Afrika.
Italia pia imesifu juhudi za Algeria za kupambana na usafirishaji haramu wa wahamiaji na biashara ya binadamu, na kusema: Imeridhishwa na kiwango cha sasa cha ushirikiano wa pande mbili katika kuyapatia ufumbuzi masuala hayo.
Mawaziri hao wawili aidha wamekubaliana kupanua ushirikiano katika masuala ya polisi, mafunzo, kubadilishana utaalamu na mifumo ya pamoja ya utendaji ili kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Algeria na Italia.
Algeria na Italia zinashirikiana katika masuala ya usalama kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi hizo yaliyotiwa saini mwaka 1999, kuhusu wahamiaji haramu na kuwarejesha makwao wahamiaji wasio na nyaraka vibali halali.
Idadi ndogo ya wahamiaji wa Algeria wasio na vibali halali wamekuwa wakiwasili katika kisiwa cha Sardinia cha Italia kutoka pwani ya mashariki ya Algeria.