Ramadhani, Dhifa ya Mwenyezi Mungu (9)
Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kama mvua laini ya msimu wa kuchipua inayonyeshea jangwa kavu na lenye kiu. Hebu na tuyaloweshe majangwa ya roho zetu kwa mvua hii yenye uhai.
Mwezi huu ni fursa adhimu ya kujiondoa katika mawazo yenye wasiwasi na matatizo ya maisha. Ingawa nyakati za nuru za Ramadhani hupita haraka, muda huu wa thamani hutufanya tukumbuke ahadi yetu na Mwenyezi Mungu pamoja na njia sahihi ya kuishi.
"Mwezi wa Ramadhani ambao ndani yake imeteremshwa Qur'ani kuwa mwongozo kwa watu na dalili zilizo wazi za mwongozo na upambanuzi."
Karibuni kwenye sehemu ya tisa ya kipindi cha "Dhifa ya Mwenyezi Mungu" ambacho ni kipindi maalumu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Ni jambo la kupendeza kuona futari imeandaliwa, na ni la kupendeza zaidi kuwaona waumini wakiwa wanasubiri kuwadia wakati wa adhana.Ni kama kwamba Waislamu wote katika mwezi wa Ramadhani wameketi kwenye meza moja, wakisubiri adhana kuwakaribisha katika rehema za Mwenyezi Mungu. Wanajiandaa kupokea baraka na rehema zinazoamsha roho na kuijaza nuru na usafi. Karibuni tuendelee na safari yetu ya kiroho na kufaidika na baraka za mwezi huu uliojaa nuru
Katika maisha ya mwanadamu, daima kuna mielekeo miwili inayopingana, mmoja ukiwa unamwelekeza kwenye ukamilifu na mwingine kwenye maangamizi. Mwenyezi Mungu ameweka ndani ya kila mtu uwezo wa kipekee unaoweza kumfikisha kwenye kilele cha ukamilifu. Ndani ya nafsi yetu, kuna mwelekeo wa kutenda mema, lakini madhambi yanakuwa vizuizi vikubwa vinavyotufanya tupotee kutoka kwenye njia hii iliyo nyoofu. Madhambi huziba akili ya mtu na kumnyima uwezo wa kutofautisha lililo sahihi na lisilo sahihi. Mtu anaposhindwa kutambua mema na mabaya, huanguka katika mtego wa matamanio na kupotea kutoka kwenye njia sahihi.
Madhambi hayadhuru roho na nafsi tu, bali yanaathiri pia uhusiano wa kijamii. Matatizo mengi katika jamii yanatokana na kupuuza amri za Mwenyezi Mungu na kufanya madhambi. Madhambi yana athari mbaya, na tutazungumzia baadhi yake hapa.
Mwanafasihi mashuhuri wa Kiirani, Mowlavi, katika kisa kilichojaa hekima na mafunzo, anazungumzia kadhia hii kwa kusema: " Mtu mmoja alikuwa akienda jangwani kila siku kukata miiba ili kujipatia riziki. Siku moja, akajiuliza kwa nini ajisumbue kwenda jangwani kila siku? Akaamua kupanda miiba karibu na nyumba yake ili asiende mbali tena. Kadri siku zilivyopita, miiba ilikua na kuanza kuwaumiza watu waliopita karibu na nyumba yake. Watu walimshauri aikate, lakini akaendelea kuahirisha. Hatimaye, kiongozi wa mji alimwambia: "Kumbuka kwamba kadri siku zinavyopita, mizizi ya miiba inakuwa migumu zaidi na wewe unazidi kuzeeka na kudhoofika." Hadithi hii ni funzo kwamba tunapokuwa na nguvu bado tuna nafasi ya kuondoa tabia mbaya, lakini tukiruhusu zishamiri, zinakuwa vigumu kuziondoa. Hivyo, ni lazima tujilinde dhidi ya madhambi yasije yakachukua mizizi katika nyoyo zetu na kutufanya tuwe mbali na nuru ya mwongozo wa Mwenyezi Mungu.
Mojawapo ya madhara ya madhambi ni kupungua kwa baraka. Maisha ya mwanadamu yamejaa baraka na neema za Mwenyezi Mungu, lakini madhambi na kupotoka kutoka njia sahihi hupelekea kupungua kwa neema hizi. Qur'ani inasema wazi kuwa binadamu anapotumia neema vibaya, kwa israfu au kwa njia mbaya, Mwenyezi Mungu huiondoa neema hiyo ili kumhimiza atubu na arejee kwenye uongofu.
Mmoja wa masahaba mwenye heshima wa Amiri wa Waumini, Imam Ali (AS), alikuwa na mtukufu huyo alipoona mtu akilalamika kuhusu ukame na uhaba wa maji. Imam, kwa huruma kubwa, alimsihi atubu na kumuomba msamaha Mwenyezi Mungu. Mtu mwingine pia alikuja akilalamika kuhusu umaskini na hali ngumu ya maisha, na Imam alimpa ushauri ule ule.
Wakati Imam alpoulizwa kwa nini alitoa ushauri huo, alijibu kwa hekima na ufahamu akisema: "Hii ni kauli ya Mwenyezi Mungu kama ilivyo katika aya ya 52 ya Suratul Hud, ambapo Nabii Hud aliwaambia watu wake: Na enyi watu wangu! Muombeni msamaha Mola wenu Mlezi, kisha mtubie kwake. Atakuleteeni mbingu zenye kunyesha mvua ya kumiminika, na atakuzidishieni nguvu juu ya nguvu zenu. Wala msigeuke mkawa wakosefu. "
Madhara mengine ya madhambi ni ugumu wa moyo. Wale wanaoendelea kuzama katika madhambi hupoteza utulivu wa ndani na uhusiano wao na Mwenyezi Mungu hufifia. Hata hivyo, si kila mwenye kutenda dhambi ni mpuuzaji au mwenye kutojali; wengine hupata hisia ya majuto baada ya kutenda dhambi huku wakihisi mzigo mzito ndani ya nafsi zao. Hii ni dalili kwamba bado kuna nafasi ya kurejea kwa Mwenyezi Mungu.
Uislamu unatoa njia bora ya kuondokana na madhara ya madhambi ambayo ni toba.
Naam, toba si tu kwamba husafisha roho kutoka kwenye dhambi, bali pia husaidia kuzuia madhambi yajayo na kurekebisha tabia ya mtu.
Imam Ali (AS), katika moja ya kauli zake zilizojaa hekima alisema: "Usiwe kama mtu anayetaka wokovu wa Akhera lakini hafanyi lolote kwa ajili ya kufikia lengo hilo, anayejua njia aliyomo si sahihi lakini hairekebishi, anayewapenda watu wema lakini hatendi kama wao, na anayechukia watenda madhambi lakini anatenda madhambi."
Maneno haya yanatufundisha kuwa matarajio mema bila juhudi hayatatupeleka popote. Hebu, katika mwezi huu wa rehema na msamaha, tusisite kutubu na kumwomba Mwenyezi Mungu atusafishe nyoyo zetu kutoka dhambini na kutuweka pamoja na watu wema.
Tunaendeleza makala yetu kwa kusikiliza dua ya siku ya tisa ya Mwezi Mtukufu Ramadhani inayosomeka hivi.
"Ee Mwenyezi Mungu! Nipe sehemu ya rehema yako iliyo pana, niongoze kwenye nuru ya hoja zako, na uniongoze kwenye ridhaa yako kwa upendo wako. Ee Mwenyezi Mungu, tumaini la wanaokutafuta!"
Katika dua ya siku ya tisa ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, tunamuomba Mwenyezi Mungu atufanikishe kwa rehema zake zilizoenea kila mahali. Hakika Mwenyezi Mungu humpatia kila kiumbe wake rehema yake, lakini kwa waja wake wema na watiifu, ameandaa rehema maalum, ambayo huwafikia duniani na Akhera. Katika dua hii, tunamwomba Mwenyezi Mungu atufanikishe kwa rehema hii maalum, na atuonyeshe dalili za wazi na hoja thabiti katika njia ya uongofu, ili tuweze daima kutembea katika njia inayompendeza Yeye.
Marafiki wapendwa, tumefikia mwisho wa sehemu ya tisa ya kipindi cha "Dhifa ya Mwenyezi Mungu". Tunatumai kuwa kipindi hiki kimekuwa chenye msukumo kwenu, na kwamba hadi sasa mmeweza kufaidika na baraka za mwezi huu uliojaa nuru. Hadi wakati mwingine panapo majaliwa yake Mola, jaribuni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa dua na ibada, na mnufaike na fursa za mwezi huu mtukufu.
Tunawaombea nyote uongofu na kukubaliwa kwa ibada zetu
"Ee Mwenyezi Mungu! Nakuomba mema yote ambayo wengine wanakuomba, na unipe bora zaidi ya yale unayowapa waja wako."