Kwa nini Marekani inataka Uturuki iachane na nishati ya Russia?
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ameitaka Uturuki iache kununua nishati ya Russia.
Marco Rubio, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani katika mazungumzo na Hakan Fidan waziri mwenzake wa Uturuki mjini Washington, ameitaka Uturuki iache kununua rasilimali za nishati kutoka Russia.
Amesisitiza takwa la Rais Trump wa Marekani kwa washirika wote wa NATO kuacha kununua rasilimali za nishati kutoka Russia. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema katika taarifa Jumatatu, Novemba 10, baada ya mawaziri hao wawili kukutana mjini Washington kwamba Washington inaamini kuwa suala hilo litasaidia kumaliza vita vinavyoendelea nchini Ukraine.
Rais Donald Trump wa Marekani amezitaka mara kadhaa nchi za Ulaya na Asia kuacha kununua mafuta ya Russia. Marekani tayari imeiwekea India ushuru maradufu kwa sababu ya kununua mafuta ya Russia. Oktoba iliyopita, iliyawekea vikwazo mashirika mawili makubwa ya mafuta ya Russia, Rosneft na Lukoil, ikitaja kutokuwepo kwa maendeleo katika juhudi za kutatua mzozo wa Ukraine.
Kwa ujumla, sanjari na ongezeko kubwa la mashinikizo dhidi ya Moscow, Washington inataka kupunguza utegemezi wa Uturuki kwa nishati ya Russia kwa sababu utegemezi huu unaimarisha ushawishi wa kisiasa na kiuchumi wa Moscow katika eneo, unapunguza uwezo wa Washington kutoa mashinikizo dhidi ya Russia katika vita vya Ukraine na kubana uhuru wa kimkakati wa Uturuki ndani ya mfumo wa NATO.
Sababu kuu za mashinikizo ya Marekani kwa Uturuki ili iache kununua nishati ya Russia zinaweza kuorodheshwa katika masuala yafuatayo:
- Vita vya Ukraine na mashinikizo ya kiuchumi kwa Russia:
Marekani inaamini kwamba ununuzi wa mafuta na gesi ya Russia unaofanywa na washirika wa NATO, ikiwa ni pamoja na Uturuki, unaipatia Kremlin rasilimali muhimu za kifedha kwa ajili ya kuendeleza vita nchini Ukraine. Washington imesisitiza mara kwa mara kwamba kusimamisha ununuzi wa nishati ya Russia kunaweza kusaidia kudhoofisha uchumi wa nchi hiyo na hivyo, kupunguza nguvu zake za kijeshi.
- Kupunguza ushawishi wa kijiopolitiki wa Russia nchini Uturuki:
Russia imekuwa mdhamini mkuu wa gesi ya Uturuki, ambapo licha ya kupungua uuzaji wa gesi hiyo katika miongo miwili iliyopita kutoka zaidi ya asilimia 60 hadi karibu asilimia 37 kufikia mwaka huu wa 2025, lakini bado ina nafasi muhimu katika kuidhaminia Uturuki gesi yake ya matumizi. Marekani inataka utegemezi huu upunguzwe zaidi ili Russia isiweze kutumia nishati kama chombo cha mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Ankara.
- Ushirikiano wa Uturuki na NATO na Magharibi:
Uturuki ni mwanachama wa NATO na Washington inatarajia nchi hii kwenda sambamba na Magharibi kuhusu siasa zake za nishati. Kuendelea kununuliwa nishati ya Russia na Uturuki kunaunda aina fulani ya pengo katika muungano wa NATO na kuipa Russia fursa ya kudumisha uhusiano maalum na Ankara.
- Kutumika vyanzo mbadala vya nishati:
Marekani na washirika wake wanajaribu kuishinikiza Uturuki iagize nishati kutoka vyanzo mbadala, ikiwa ni pamoja na gesi asilia ya Marekani (LNG) na kuongeza uzalishaji wa ndani ya nchi. Inatabiriwa kuwa ifikapo mwaka 2028, Uturuki itakuwa na uwezo wa kuzalisha nusu ya mahitaji yake ya gesi bila kuitegemea Russia.
- Kufungamana na sera ya vikwazo:
Marekani imeweka vikwazo vikubwa dhidi ya makampuni ya mafuta ya Russia kama vile Rosneft na Lukoil. Ikiwa Uturuki itaendelea kununua nishati ya Russia, vikwazo hivi havitakuwa na taathira kubwa ambapo Russia itakuwa imepata njia muwafaka ya kukwepa mashinikizo ya kiuchumi.
Mambo yanayopewa Umuhimu na Uturuki
Hii ni katika hali ambayo ni vigumu sana kwa Ankara kutoa jibu chanya kwa ombi la Marekani la kupunguza uhusiano wake na Moscow, hasa la kuacha kunufaika na nishati ya Russia. Mbali na nishati, Uturuki pia inashirikiana na Russia katika nyanja za kijeshi, kama vile ununuzi wa mfumo wa ulinzi wa anga wa S-400. Mahusiano ya kiuchumi na kibiashara kati ya Moscow na Ankara pia ni makubwa sana. Kampuni ya Rosatom pia imejenga kiwanda cha kwanza cha nyuklia cha Uturuki, kinachojulikana kama "Akkuyu". Mradi huu mkubwa uliojengwa kwenye pwani ya Mediterania kwa msingi wa teknolojia ya Russia na unaosimamiwa na kuendeshwa na wataalamu wa nchi hiyo, unapitia hatua zake za mwisho za ujenzi.
Hata hivyo, Marekani inadai kuwa uhusiano wa Moscow na Ankara unatishia mshikamano wa NATO, hivyo inajaribu kupunguza wigo wa ushirikiano wa kimkakati kati ya Uturuki na Russia kwa kuweka mashinikizo kwenye sekta ya nishati ya nchi mbili. Ingawa kufutwa nishati ya Russia ni gharama kubwa kwa Uturuki, Marekani inaiona kama fursa ya kubadilisha vyanzo vya nishati na kupunguza hatari za kijiopolitiki, na kudai kuwa mabadiliko haya yanaweza kuimarisha usalama wa nishati kwa Uturuki katika kipidi cha muda mrefu. Ikizingatiwa kuwa Uturuki iliyo kati ya Ulaya na Asia ina mchango mkubwa katika usafirishaji wa nishati, Marekani inadai kuwa iwapo nchi hii itajitenga na nishati ya Russia, njia mbadala za usafirishaji wa nishati kutoka Asia Magharibi na Asia ya Kati kwenda Ulaya zitaimarishwa na hivyo kupunguza utegemezi wa Ulaya kwa nishati ya Russia.
Muhtasari
Marekani inataka Uturuki iache kununua nishati ya Russia ili kubana matumizi ya kifedha ya nchi hiyo katika vita vya Ukraine, kupunguza ushawishi wa kisiasa wa Moscow kwa Ankara, kuimarisha muungano wa NATO na kuanzisha njia mbadala za nishati kwa Ulaya. Sera hii ni sehemu ya mkakati mkuu wa Washington wa kuidhibiti Russia na kudhamini usalama wa nishati kwa washirika wake wa Magharibi.