India, Russia zasisitiza utatuzi wa mpango wa nyuklia wa Iran kupitia mazungumzo
-
India, Russia zasisitiza utatuzi wa mpango wa nyuklia wa Iran kupitia mazungumzo
Baada ya Rais wa Russia Vladimir Putin na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi kukutana mjini New Delhi, nchi hizo mbili zimesisitiza umuhimu wa kutatua masuala yanayohusiana na mpango wa nyuklia wa Iran kwa njia ya mazungumzo.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa jana Ijumaa baada ya mkutano kati ya Rais wa Russia Vladimir Putin na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi mjini New Delhi, Russia na India zimetoa wito wa kujizuia na kuheshimu haki za binadamu Asia Magharibi na kusisitiza umuhimu wa kutatuliwa mpango wa nyuklia wa Iran kwa njia ya mazungumzo.
Russia na India zimeelezea wasiwasi wao kuhusu hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa mikataba ya amani ili kumaliza mzozo katika Ukanda huo.
Russia na India pia zimetoa wito wa kufanyiwa marekebisho kamili muundo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na Moscow ikatangaza kuunga mkono India kugombea uanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Putin pia alisema katika mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari na Modi: Russia na India hufuata sera huru ya kigeni na kushirikiana ndani ya mfumo wa BRICS na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai kuunda utaratibu wa pande nyingi zaidi, wa kidemokrasia na wa haki.
Mazungumzo ya Putin na Modi yamefanyika huku utawala wa Marekani ukiongozwa na Donald Trump ukiishutumu Russia kwa kuendelea kusafirisha mafuta nchini India kama njia ya "kufadhili vita vya Putin nchini Ukraine" na kuweka ushuru wa asilimia 50 kwa bidhaa nyingi za India mwezi Agosti. Licha ya shinikizo hizi, New Delhi imesisitiza kudumisha uhuru wake katika uwanja wa biashara.