Zambia yaelekea kwenye uchaguzi; Rais Hichilema anawania muhula wa pili
-
Zambia katika uchaguzi wa Rais Agosti 13
Watu wa Zambia leo Alhamisi wanashiriki katika uchaguzi ili kuamua iwapo Rais Hakainde Hichilema atapata muhula wa pili wa miaka mitano kama zawadi ya mpango wake wa ufufuzi wa uchumi katika taifa hilo la Kusini mwa Afrika, ambalo ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa shaba duniani lakini lilikumbwa na mgogoro wa madeni hivi karibuni.
Hichilema alishinda uchaguzi wa rais mwaka 2021, baada ya kushindwa katika majaribio matano ya awali kuanzia mwaka 2006.
Katika kinyang’anyiro chenye wagombea wengine 13 wa urais, wachambuzi wanasema mpinzani mkuu wa Hichilema huenda akawa Brian Mundubile, kiongozi wa muungano wa upinzani uitwao Tonse Alliance. Mundubile mwenye umri wa miaka 55, ambaye ni mhitimu wa sheria, hakuonekana kuwa kiongozi mkuu wa kisiasa nchini Zambia hadi alipoibuka Januari mwaka huu kama kiongozi wa Tonse kufuatia mgogoro wa ndani ya muungano huo.
Ingawa mfumuko wa bei umeshuka na thamani ya sarafu ya Zambia, Kwacha, imeimarika chini ya uongozi wa Hichilema, wananchi wa kawaida wanalalamikia gharama kubwa ya chakula na nishati.
Wakosoaji wengine wanasema utulivu wa jumla wa uchumi haujawanufaisha watu wengi katika nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 22.
Zambia ilijinyakulia uhuru kutoka Uingereza mwaka 1964 na ilikuwa nchi ya chama kimoja kutoka mwaka 1973 hadi 1991. Tangu wakati huo, vyama kadhaa na miungano ya kisiasa imekuwa ikishinda na kupoteza madaraka.
China ndiye mwekezaji mkuu wa kigeni nchini Zambia, hususan katika sekta ya shaba na kobalti, madini muhimu yanayotumiwa katika vifaa vya elektroniki, magari ya umeme, na teknolojia nyingine mpya. Madini hayo pia yamemvutia Rais Donald Trump wa Marekani. Zambia imeishutumu Marekani kwa kuhusisha upatikanaji wa madini muhimu na mkataba wa afya wa dola bilioni 2 uliopendekezwa kati ya nchi hizo. Serikali ya Hichilema imekataa kusalimu amri mbele ya matakwa ya Trump kuhusu madini.
Wapiga kura katika uchaguzi huo wa siku moja, Alhamisi, watachagua pia wabunge na madiwani wa serikali za mitaa. Takriban watu milioni 8 wamejiandikisha kupiga kura. Uchaguzi wa rais nchini Zambia unatumia mfumo wa “asilimia 50 pamoja na kura moja,” ambapo mgombea lazima apate kura nyingi zaidi ili kushinda. Hali hii inaleta uwezekano wa raundi ya pili ya kupiga kura ikiwa hakuna mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura katika awamu ya kwanza.