Bunge la Zimbabwe lajadili rasimu ya muswada wa kuongeza muda wa urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138854-bunge_la_zimbabwe_lajadili_rasimu_ya_muswada_wa_kuongeza_muda_wa_urais
Bunge la Zimbabwe linazingatia muswada tata wa marekebisho ya Katiba ambao utaongeza muhula wa Rais Emmerson Mnangagwa kwa miaka miwili hadi 2030.
(last modified 2026-06-03T12:39:58+00:00 )
Jun 03, 2026 12:35 UTC
  • Emmerson Mnangagwa
    Emmerson Mnangagwa

Bunge la Zimbabwe linazingatia muswada tata wa marekebisho ya Katiba ambao utaongeza muhula wa Rais Emmerson Mnangagwa kwa miaka miwili hadi 2030.

Pia marekebisho hayo yatafuta Uchaguzi Mkuu wa Rais, na kulipa Bunge mamlaka ya kumteua mkuu wa nchi.

Zaidi ya hayo, mabadiliko yaliyopendekezwa, yaliyowasilishwa na Waziri wa Sheria Ziyambi Ziyambi katika Bunge la Chini siku ya Jumanne, yataruhusu wabunge kuongezwa muda wao kutoka miaka mitano hadi saba.

Waziri Ziyambi amesema mchakato wa mashauriano ya umma wa siku 90 ulifanikiwa na uliungwa mkono pakubwa.

Hata hivyo, wapinzani wanasema uligubikwa na vitisho na vurugu, huku wanaharakati wanaopinga marekebisho hayo wakishambuliwa na watu wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na serikali au kukamatwa.

Changamoto kadhaa za kisheria zinazotaka kusimamisha au kubatilisha mchakato wa marekebisho ya Katiba kwa sasa ziko mbele ya mahakama za Zimbabwe.

Wachambuzi wa siasa wanasema wanatarajia muswada huo kupitishwa katika Bunge la Chini ambapo chama cha Mnangagwa cha ZANU-PF kina wingi wa theluthi mbili.

Wakosoaji wanasema marekebisho hayo yataimarisha udhibiti wa chama cha Zanu-PF, ambacho kimetawala nchi hiyo yenye utajiri wa rasilimali tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1980.

Mnangagwa aliingia madarakani mwaka wa 2017 katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na jeshi yaliyomng'oa madarakani Robert Mugabe ambaye alikuwa rais wa Zimbabwe kwa kipindi cha miaka 30.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 83 alichaguliwa kwa mihula miwili ya miaka mitano, mwaka 2018 na 2023, ambayo ni kikomo cha kikatiba kwa rais.

Muda wa kuwa kwake madarakani umeandamana na madai ya ukandamizaji wa kisiasa, kuoza kwa taasisi za serikali na mgogoro mkubwa wa kiuchumi.