Mazuwari zaidi ya milioni nne wameingia Iraq tangu Muharram hadi sasa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140354-mazuwari_zaidi_ya_milioni_nne_wameingia_iraq_tangu_muharram_hadi_sasa
Mkuu wa Idara ya habari ya masuala ya usalama wa Iraq ametangaza kuwa wafanyaziara zaidi ya milioni nne wa kigeni wamewasili nchini humo tangu mwanzo wa mwezi wa Muharram, na kwamba zoezi la upokeaji mazuwari wanaokwenda kushiriki kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein AS lingali unaendelea.
(last modified 2026-08-02T03:29:40+00:00 )
Aug 02, 2026 03:27 UTC
  • Mamilioni ya Waislamu wamewasili Karbala kwa Ziara ya Arubaini ya Imam Hussein (as).
    Mamilioni ya Waislamu wamewasili Karbala kwa Ziara ya Arubaini ya Imam Hussein (as).

Mkuu wa Idara ya habari ya masuala ya usalama wa Iraq ametangaza kuwa wafanyaziara zaidi ya milioni nne wa kigeni wamewasili nchini humo tangu mwanzo wa mwezi wa Muharram, na kwamba zoezi la upokeaji mazuwari wanaokwenda kushiriki kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein AS lingali unaendelea.

Saad Maan amesema: takwimu rasmi kutoka taasisi husika zinaonyesha kuwa kuanzia siku ya kwanza ya mwezi wa Muharram hadi Ijumaa jioni, mazuwari wa kigeni milioni nne elfu 7,257 wameingia Iraq.

Akizungumza na Shirika la Habari la Shafaq, Maan ameendelea kueleza kuwa takwimu hizo zimetokana na ripoti rasmi za vyombo husika na kwamba kuna uwezekano wa kuongezeka katika siku zijazo mazuwari watapoendelea kuwasili.

Kabla ya hapo, Tume Kuu ya Usimamizi wa Ziara ya Arubaini katika Ofisi ya Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Iraq ilitangaza siku ya Alkhamisi iliyopita kwamba, kwa mujibu wa takwimu zilizosasishwa, wafanyaziara milioni 2, 887 elfu 305 wameingia Iraq tangu mwanzo wa Muharram hadi Jumatano jioni; takwimu ambazo sasa zimefikia zaidi ya watu milioni nne huku mazuwari wakiendelea kuwasili ili kushiriki kwenye kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein AS katika mji mtakatifu wa Karbala.

Kila mwaka, na katika siku ya arubaini baada ya Ashura, Waislamu wa madhehebu ya Shia huadhimisha kuuawa shahidi Imam Hussein AS na masahaba zake katika tukio la Karbala lililojiri mwaka wa 61 Hijria kwa kushiriki katika matembezi na hafla ya Arubaini.

Matembezi ya Arubaini hufanyika katika siku zinazokaribia tarehe 20 Safar kwa mazuwari kuelekea Karbala kwa lengo la kufanya ziara ya Arubaini. Matembezi hayo hufanywa kutokea sehemu mbalimbali za Iraq na baadhi ya miji ya Iran. Wafanyaziara wengi wa Kiirani na wanaotoka nchi kama vile Pakistan hutembea kwa miguu kutoka Najaf hadi Karbala masafa ya takribani kilomita 80. Katika njia yanakopitia matembezi hayo, kuna vituo vya kuwakirimu mazuwari, ambavyo vinajulikana kama Mawaakib.

Katika miaka ya karibuni, mamilioni ya watu kutoka pembe mbalimbali za dunia wameshiriki katika Matembezi ya Arubaini na kulifanya tukio hilo kuwa mkusanyiko mkubwa zaidi wa kidini wa kila mwaka duniani…/