Trump na mkakati wa kuchochea ubaguzi wa rangi
Donald Trump, Rais wa Marekani, ameendeleza mashambulizi makali dhidi ya wahamiaji wa Kisomali akisema: “Somalia inanuka.” Aidha, alimueleza Ilhan Omar, mbunge wa Kidemokrasia na Mwislamu, kuwa ni “takataka.”
Kwa mujibu wa taarifa, kauli hizi zilitolewa mwishoni mwa kikao cha baraza la mawaziri, zikilenga moja kwa moja jamii ya Kisomali wanaoishi Marekani. Maneno haya yanaonyesha mwendelezo wa siasa zake za kupinga uhamiaji na ni kielelezo cha wazi cha ghasia za kisiasa zenye misingi ya ubaguzi wa rangi.
Kwa hakika, matamshi ya Trump si matusi ya kawaida tu, bali ni sehemu ya mkakati mpana wa kisiasa unaojengwa juu ya misingi ya ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa kidini na uchochezi wa hisia za kupinga wahamiaji.
Donald Trump kwa mara nyingine ameonyesha kuwa ubaguzi wa rangi kwake si kosa la lugha au tusi la binafsi, bali ni moja ya nguzo kuu za mkakati wake wa kisiasa. Wakati Rais wa Marekani katika kikao cha baraza la mawaziri anapoitaja Somalia kuwa nchi yenye “harufu mbaya” na kumdhalilisha Ilhan Omar, mbunge Mwislamu wa Kongresi, kwa kumuita “takataka”, kwa hakika anatuma ujumbe wa moja kwa moja kwa ngome yake ya kisiasa: wahamiaji, Waislamu na watu wenye asili ya Afrika ni maadui wanaopaswa kusukumwa pembezoni.
Kauli hizi ni sehemu ya mradi wa kisiasa uliojengwa juu ya misingi ya kuwatenga na kuwakataa wengine, mradi unaolenga kufafanua upya utambulisho wa Marekani kwa njia ya kuondoa makundi yasiyo ya wazungu.
Siasa hizi zinajitokeza katika mazingira ambapo viongozi wa Marekani mara kwa mara hudai kuwa wanaheshimu haki sawa na kuendeleza uhuru wa kisiasa, kiuchumi na kijamii ndani ya nchi yao. Wakati huohuo, Marekani imekuwa ikizilaumu nchi nyingi kwa madai ya kukiuka haki za binadamu na kukosa uhuru, kisha kuziwekea vikwazo vya kisiasa, kijamii na kiuchumi kama adhabu.
Kutoka katika mtazamo mwingine, tangu mwanzo wa kuingia kwake katika siasa, Donald Trump ameitumia chuki dhidi ya wahamiaji kama chombo cha kuhamasisha wapiga kura wake. Kupitia lugha ya kudhalilisha dhidi ya jamii za Kiafrika na Waislamu, amebadilisha hofu na chuki kuwa mtaji wa kisiasa.
Kufutwa kwa hadhi ya ulinzi wa raia wa Kisomali walioko Minnesota, vikwazo vya kuingia kwa Waislamu, na sasa mashambulizi ya wazi ya maneno, vyote ni sehemu ya mradi wa kisiasa unaolenga kuimarisha utambulisho wa Marekani kwa msingi wa umiliki wa wazungu peke yao.
Shambulizi la moja kwa moja dhidi ya Ilhan Omar linaonyesha kuwa Trump amemchagua kama alama ya mhamiaji Mwislamu na mwanamke mweusi ili kufikisha ujumbe kwa ngome yake ya kisiasa. Omar, ambaye aliingia Marekani mwaka 2000 kama mkimbizi na sasa ni raia wa nchi hiyo, mara nyingi amekuwa shabaha ya mashambulizi ya kibinafsi na ya kudhalilisha. Hata katika mkutano wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2025, Trump alimtaja kuwa tishio kwa usalama wa taifa.
Kukariri matamshi haya kunaonyesha wazi kuwa mashambulizi dhidi ya Ilhan Omar ni sehemu ya mkakati wa kudumu na si tukio la muda mfupi. Ripoti kutoka jimbo la Minnesota zinaonyesha kuwa baada ya kauli za Trump dhidi ya wahamiaji wa Kisomali, vitisho vya kikatili dhidi ya jamii hiyo viliongezeka.
Kwa kumtaja mhamiaji kama “mzigo wa ziada” na “tishio kwa usalama wa mitaa”, Trump kwa hakika anawageuza wahamiaji kuwa adui wa ndani. Mtazamo huu unazidisha mpasuko wa kijamii na kuisukuma siasa ya Marekani kuelekea katika hali hatari ya mgawanyiko wa kisiasa.
Kutoka upande mwingine, vipengele vya kimataifa vya suala hili navyo ni vya kuzingatiwa. Wakati Rais wa Marekani anapoitaja nchi fulani kuwa yenye “harufu mbaya”, maneno haya hayabaki tu kwa wahamiaji wa taifa hilo, bali pia yanaathiri moja kwa moja uhusiano wa kidiplomasia wa Washington na mataifa ya Kiafrika pamoja na ulimwengu wa Kiislamu.
Kauli kama hizi zinaweza kusababisha kupungua kwa imani ya pande zote, kuongezeka kwa mvutano wa kidiplomasia na hata kudhoofisha nafasi ya Marekani katika taasisi za kimataifa. Mataifa ya Kiafrika huzitafsiri kauli hizi kama dharau ya moja kwa moja kwa mamlaka na heshima ya kitaifa, na hivyo majibu ya kukataa hayatakuwa na budi.
Katika dunia ambayo kwa sasa inahitaji mshikamano na imani kuliko wakati wowote, misimamo kama hii inaisukuma Marekani zaidi katika mvutano wa ndani na kuelekea katika kuporomoka kwa imani ya kimataifa.
Kwa hakika, misimamo ya kibaguzi kama hii si tu kwamba yenyewe hunuka, bali pia husambaza harufu ya hatari. Hatari hii huanzia katika kauli za rais na inaweza kugeuka kuwa ghasia za ndani, mpasuko wa kijamii na hata mgogoro wa kidiplomasia. Mwisho wa njia hii si nguvu zaidi, bali ni mgogoro mkubwa zaidi kwa jamii inayojitambulisha kama “taifa la wahamiaji.”