Hamas: Mwisho wa Abu Shabab ndio hatima isiyoepukika ya kila msaliti
-
Yasser Abu Shabab
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeonya kwamba mauaji ya mshirika wa Israel na kiongozi wa genge lenye uhusiano na Daesh, Yasser Abu Shabab, ni hatima isiyoepukika ya kila mtu anayechagua kulisaliti taifa na nchi yake na kushirikiana na utawala ghasibu wa Israel.
Redio ya jeshi la Israel ilitangaza jana Alhamisi kwamba Abu Shabab ameuawa na kundi la watu wenye silaha ambalo halijatambuliwa huko Rafah kusini mwa Gaza, eneo ambalo kwa sasa linadhibitiwa kamili na Israel.
Katika taarifa yake kuhusiana na tukio hilo, harakati ya Hamas imesema kwamba utawala wa Israel umeshindwa kuwalinda maajenti wake, ikisisitiza kwamba hatima ya mtu yeyote anayehatarisha usalama wa watu wake na kumtumikia adui wao ni "kuanguka kwenye jaa la takataka la historia na kupoteza heshima."
Harakati hiyo imeashiria umuhimu wa kuwepo umoja na mshikamano miongoni mwa watu wa Palestina ili kuzuia njama za Israel, ikizipongeza familia, makabila na koo zilizomkana Abu Shabab na washirika wake.
Taarifa ya Hamas imesema vitendo vya uhalifu vilivyofanywa na Abu Shabab na kundi lake kwa kushirikiana na jeshi la Israel "ni kielelezo cha kujivua utambulisho wa kitaifa na kijamii" na havina uhusiano wowote na maadili na mila za watu wa Palestina.
Abu Shabab aliibuka wakati wa vita vya mauaji ya kimbari vya miaka miwili kama mkuu wa kile kilichoitwa Vikosi vya Wananchi, akipora misaada na kuwaua au kuwateka nyara raia wa Palestina na wapiganaji wa Hamas pamoja na kushirikiana na vikosi vya jeshi la kizayuni.
Aliandamwa na lawama nyingi kutoka makundi ya Wapalestina, ambao walimuona yeye na kundi lake kama wasaliti na kulihusisha na Israel na Daesh.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu hapo awali alikiri kwamba genge la Abu Shabab limepewa na silaha kutoka Israel.
Chanzo cha habari cha Palestina pia kiliiambia Kan News mwezi uliopita kwamba, washirika wa Abu Shabab walishiriki katika mikutano na maafisa wakuu wa serikali Marekani.