Guinea-Bissau yasitisha utafiti wa chanjo unaofadhiliwa na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136872-guinea_bissau_yasitisha_utafiti_wa_chanjo_unaofadhiliwa_na_marekani
Guinea-Bissau imesitisha utafiti tata wa chanjo ya homa ya ini aina ya B (Hepatitis B) uliokuwa ukifadhiliwa na utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump, baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kueleza wasiwasi mkubwa wa kimaadili kuhusu muundo wa utafiti huo.
(last modified 2026-02-21T07:37:22+00:00 )
Feb 21, 2026 07:37 UTC
  • Guinea-Bissau yasitisha utafiti wa chanjo unaofadhiliwa na Marekani

Guinea-Bissau imesitisha utafiti tata wa chanjo ya homa ya ini aina ya B (Hepatitis B) uliokuwa ukifadhiliwa na utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump, baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kueleza wasiwasi mkubwa wa kimaadili kuhusu muundo wa utafiti huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa taifa hilo la Afrika Magharibi, Joao Bernardo Vieira, amesema serikali imesimamisha rasmi jaribio hilo wiki hii kufuatia wasiwasi uliotolewa na WHO.

Waziri wa zamani wa Afya wa Guinea-Bissau, Magda Robalo, alikuwa mkosoaji mkubwa wa mradi huo. Aliliambia jarida la kisayansi Nature mwezi uliopita kuwa jaribio hilo “halikubaliki na halipaswi kuendelea.”

Utafiti huo, uliokuwa ukifadhiliwa kwa ruzuku ya dola milioni 1.6 kutoka Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC), ulikusudiwa kuhusisha takriban watoto wachanga 14,000 nchini Guinea-Bissau, nchi ambayo viwango vya maambukizi ya homa ya ini aina ya B ni miongoni mwa vya juu zaidi duniani.

Kwa mujibu wa mpango wa utafiti huo, baadhi ya watoto wachanga wangepewa chanjo mara tu baada ya kuzaliwa, huku wengine wakipata chanjo hiyo baada ya wiki sita. Mabadiliko haya ya ratiba yaliungwa mkono na baadhi ya watafiti, lakini yalizua utata mkubwa kwa sababu yangesababisha kunyimwa chanjo nusu ya watoto wakati wa kuzaliwa.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa iliyopita, WHO ililaani jaribio hilo kama “lisilo la kimaadili,” ikionya kuwa kunyimwa chanjo hiyo kunaweza kusababisha “madhara yasiyoweza kurekebishwa.”

Shirika hilo la afya duniani lilielezea chanjo ya dozi ya wakati wa kuzaliwa kuwa ni “hatua muhimu na yenye ufanisi wa afya ya umma,” likibainisha kuwa kwa zaidi ya miongo mitatu, chanjo hiyo imezuia kati ya asilimia 70 hadi 95 ya maambukizi ya homa ya ini kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Hata hivyo, watafiti kutoka Mradi wa Afya wa Bandim ulioko Guinea-Bissau, unaosimamiwa na Chuo Kikuu cha Southern Denmark, walitetea malengo ya kisayansi ya utafiti huo. Frederik Schaltz‑Buchholzer, mtafiti mkuu wa mradi huo, alisema mjadala huo umegeuka zaidi kuwa wa kisiasa kuliko wa kisayansi.

Mkurugenzi Mkuu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Jean Kaseya, amesema mamlaka za afya barani Afrika lazima zibaki na udhibiti kamili wa tafiti zote zinazofanywa ndani ya bara hilo.