WFP: Somalia inakabiliwa na hatari ya baa la njaa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136870-wfp_somalia_inakabiliwa_na_hatari_ya_baa_la_njaa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limesema hali ya upatikanaji wa chakula nchini Somalia imefikia hatua mbaya ambapo mamilioni ya watu wako hatarini kukumbwa na njaa kali kutokana na ukosefu wa fedha za msaada.
(last modified 2026-02-21T07:36:21+00:00 )
Feb 21, 2026 07:36 UTC
  • WFP: Somalia inakabiliwa na hatari ya baa la njaa

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limesema hali ya upatikanaji wa chakula nchini Somalia imefikia hatua mbaya ambapo mamilioni ya watu wako hatarini kukumbwa na njaa kali kutokana na ukosefu wa fedha za msaada.

Taarifa ya WFP iliyotolewa Ijumaa huko Mogadishu nchini Somalia, imesema wa sasa, watu milioni 4.4 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku karibu milioni moja kati yao wakiteseka kwa njaa kali.

Hali ya ukata ikiendelea, WFP imeonya kuwa huduma zake za dharura za chakula na lishe mjini Mogadishu na maeneo mengine zinaweza kusitishwa ndani ya wiki chache zijazo ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.

Hatua hii imekuja baada ya nchi hiyo kutangaza hali ya dharura ya ukame kufuatia kukosekana kwa mvua kwa misimu miwili mfululizo, jambo lililosababisha vifo vya mifugo na uharibifu wa mazao.

Ross Smith, ambaye ni Mkurugenzi wa WFP anayehusika na maandalizi ya kukabili dharura, amebainisha kuwa hali inazidi kuwa mbaya kwa kasi ya kutisha na familia nyingi zimepoteza kila kitu.

Amesema: "Hali inaharibika kwa kasi ya kutisha. Bila msaada wa chakula wa dharura hivi sasa, hali itazidi kuwa mbaya zaidi. Tuko kwenye wakati mgumu; bila hatua za haraka, tunaweza kushindwa kuwafikia watu walio hatarini zaidi kwa wakati, wengi wao wakiwa wanawake na Watoto."

Kutokana na upungufu mkubwa wa fedha, tayari WFP imelazimika kupunguza idadi ya watu wanaopata msaada kutoka milioni 2.2 mwanzoni mwa mwaka 2025 hadi kufikia watu 600,000 pekee.

Hii inamaanisha kuwa kwa sasa shirika hilo linamsaidia mtu mmoja tu kati ya kila watu saba wenye uhitaji mkubwa wa chakula.

Vilevile, mipango ya lishe kwa ajili ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha imepunguzwa kwa kiasi kikubwa, jambo ambalo limeongeza hofu ya kuongezeka kwa utapiamlo kwa watoto wadogo nchini humo.

Ross Smith amekumbushia mafanikio ya mwaka 2022 ambapo njaa kama hii iliepukwa kupitia msaada wa kimataifa, akisisitiza kuwa shirika linao uwezo wa kutoa huduma iwapo rasilimali zitapatikana.

Shirika hilo linahitaji kiasi cha dola milioni 95 za Marekani ili kuendelea kusaidia watu wenye uhitaji kuanzia mwezi Machi hadi Agosti mwaka huu.

Misaada ya kibinadamu nchini Somalia inakaribia kumalizika ambapo hatua za haraka za Jumuiya ya Kimataifa zinahitajika. WFP imeonya kuwa ikiwa fedha hazitapatikana,  italazimika kusitisha kabisa misaada yote ya kibinadamu ifikapo mwezi Aprili mwaka huu.