Nigeria inachunguza shambulio lililosababisha vifo vya watu 25 katika jimbo la Plateau
Watu wasiopungua 25 wameuawa katika shambulio dhidi ya kijiji kimoja katika jimbo la Plateau katikati mwa Nigeria.
Msemaji wa polisi katika jimbo la Plateau, Alfred Alabo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa maafisa husika walitarajiwa kutoa taarifa baada ya kufika katika eneo la tukio.
Hapo awali, jamii katika Jimbo la Plateau zimeshuhudia mivutano kati ya wakulima na wafugaji ambayo mara nyingi hugeuka kuwa vurugu za kulipiza kisasi na kusababisha vifo na kupelekea watu kuyahama makazi yao.
Lemun Le'an Iliya, diwani anayewakilisha eneo hilo palipojiri mauaji amesema kuwa watu 23 waliuawa katika shambulio hilo na majeruhi mwingine alifariki dunia baadaye hospitalini.
Kundi kwa jina la "Mwaghavul Youth Movement" limetoa wito kwa serikali ya jimbo la Plateau kuzidisha juhudi za kulinda jamii zilizo katika hatari na kupitia upya operesheni za usalama katika eneo hilo.
"Uharibifu wa mara kwa mara wa jamii, mauaji ya raia wasio na hatia, kuchomwa moto nyumba na kuharibiwa mashamba haviwezi kuendelea kuchukuliwa kama matukio ya kawaida," amebainisha msemaji wa kundi hiloTubwot Joël Sunday.
Jimbo la Plateau ambalo linapatikana katika ukanda wa 'Middle Belt' nchini Nigeria kwa muda mrefu limekmbwa na ghasia zinazohusiana na migogoro ya ardhi, haki za malisho na upatikanaji wa rasilimali; migogoro ambayo mara nyingi huchochewa zaidi na mivutano ya kikabila na kidini.