Utafiti: Vita vya Gaza vinawasukuma Waingereza kwenye dini ya Uislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i133954-utafiti_vita_vya_gaza_vinawasukuma_waingereza_kwenye_dini_ya_uislamu
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Uingereza ya Athari ya Imani katika Maisha (IIFL) umeonyesha kuwa migogoro ya kimataifa ni sababu kuu kwa Waingereza kukubali dini ya Uislamu.
(last modified 2025-12-05T10:52:32+00:00 )
Dec 05, 2025 10:52 UTC
  • Wasichana wakivuka barabara kuelekea msikitini jijini London
    Wasichana wakivuka barabara kuelekea msikitini jijini London

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Uingereza ya Athari ya Imani katika Maisha (IIFL) umeonyesha kuwa migogoro ya kimataifa ni sababu kuu kwa Waingereza kukubali dini ya Uislamu.

Watafiti waliofanya utafiti huo wamegundua kuwa matokeo yao yanaimarisha madai ya kuongezeka viwango vya watu kubadili dini na kuwa Waislamu katika kipindi cha vita vya Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Uchunguzi huo umesema kwamba, ripoti za vyombo vya habari zinazofungamanisha mazingatio ya Waingereza kwa Uislamu na migogoro inayoathiri jamii za Waislamu, zinaweza kuwa na umuhimu mkubwa.

Matokeo ya utafiti huo ambayo yamechapishwa kwenye tovuti ya taasisi hiyo, yamehitimisha kwamba vita vya dunia huwaelekeza Waingereza kwenye kukubali dini Uislamu.

Watafiti wamesema, "mwenendo huu unaweza kuungwa mkono na ripoti za vyombo vya habari zilizochapishwa mwishoni mwa 2023 na 2024, ambazo zinaonyesha ongezeko kubwa la watu waliojiunga na Uislamu kufuatia vita vya hivi karibuni vya Israel dhidi ya Gaza."

Watafiti pia wamebainisha katika ripoti yao kwamba "watu wanaosilimu mara nyingi hufanya hivyo wakitafuta lengo."

Kwa mujibu wa utafiti huo, 20% ya wale waliosilimu hivi karibuni wamefanya hivyo kwa sababu zinazohusiana na migogoro ya kimataifa, huku 18% wakisilimu kwa sababu zinazohusiana na afya ya akili.

Ukrisho unapungua Uingereza:

Katika muktadha huo, sensa iliyofanywa hivi karibuni na Ofisi ya Takwimu za Kitaifa ya Uingereza imebaini kuwa Wakristo sasa wanaunda chini ya nusu ya idadi ya watu wa Uingereza na Wales, ikiwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Telegraph, matokeo ya sensa yameonyesha kuwa 46.2% ya idadi ya watu (watu milioni 27.5) walijieleza kama "Wakristo" mwaka wa 2021, ikiwa ni upungufu wa 13.1% kutoka 59.3% (watu milioni 33.3) ikilinganishwa na matokeo ya utafiti kama huo mwaka wa 2011.