China yapinga uingiliaji wa Marekani katika masuala ya Venezuela
https://parstoday.ir/sw/news/world-i133900-china_yapinga_uingiliaji_wa_marekani_katika_masuala_ya_venezuela
Serikali ya China imetangaza kuwa, inapinga vikali uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela.
(last modified 2025-12-04T04:04:36+00:00 )
Dec 04, 2025 04:04 UTC
  • China yapinga uingiliaji wa Marekani katika masuala ya Venezuela
    China yapinga uingiliaji wa Marekani katika masuala ya Venezuela

Serikali ya China imetangaza kuwa, inapinga vikali uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela.

Kufuatia kuongezeka vitisho vya Washington dhidi ya Caracas, Wizara ya Mambo ya Nje ya China imepinga uingiliaji wa kigeni kwa kisingizio chochote katika masuala ya ndani ya Venezuela.

Kufuatia kupanuka kwa operesheni na harakati za kijeshi za Marekani katika eneo la Caribbean na tishio la kufungwa anga ya Venezuela, jambo ambalo limezidisha hali ya wasiwasi kati ya Washington na Caracas, China imepinga vikali uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya Venezuela.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Lin Jian amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing kwamba nchi yake inapinga hatua yoyote inayokiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa au kutilia shaka mamlaka ya nchi nyingine.

Lin Jian ametoa wito kwa pande zote kuchukua hatua ya kuhifadhi Amerika ya Kusini na Karibiani kama "eneo la amani" na kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.

Serikali ya Marekani imeongeza shinikizo kwa Venezuela kupitia uimarishaji wa nguvu za kijeshi katika eneo Karibiani, ikidai ni operesheni ya kupambana na biashara ya dawa za kulevya bila ushahidi wenye mashiko. Venezuela inasema hatua hizo, zinazoongozwa na Rais Donald Trump na utawala wake, zinalenga kuipindua serikali ya Maduro na kutwaa rasilimali kubwa za taifa hilo, hususan utajiri wa mafuta na dhahabu. Venezuela ina akiba kubwa zaidi ya petroli duniani.

Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, amesema Caracas haitainama mbele ya shinikizo la kijeshi na kisiasa kutoka Washington, akisisitiza taifa hilo linapinga aina yoyote ya amani ambayo ni sawa na "utumwa" kwa Marekani.