Russia: Hakuna mazungumzo ya kusitisha mapigano mkesha wa Mwaka Mpya
Msemaji wa Ikulu ya Russia, Kremlin, amesema kuwa, hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika kuhusu kusimamishwa vita wakati wa mkesha wa X-Mass na mwaka mpya huko Ukraine.
Pavel Voshchanov amesema hayo mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa, madai kwamba kuna uwezekano wa kusimamishwa vita huko Ukraine hayana ukweli na kwamba kusitisha mapigano kwenye kipindi cha Mwaka Mpya katika eneo maalumu la operesheni ni jambo ambalo hata kujadiliwa halijajadiliwa. Amesema, Russia haiungi mkono kusimamishwa vita kwa muda.
Matamshi hayo ya Msemaji wa Ikulu ya Russia yamekuja huku Rais Vladimir Putin akirudia kusema kwamba Moscow inaunga mkono makubaliano ya muda mrefu bila ya kusitisha mapigano kwa muda. Makubaliano ya muda mrefu yanawezekana tu baada ya kushughulikia mizizi ya mzozo wa Ukraine. Sababu hizo ni pamoja na vitisho kwa usalama wa taifa la Russia vinavyosababishwa na sera za kikoloni za NATO za kupanua mipaka yake. Sababu nyingine ni ukandamizaji wanaofanyiwa watu wanaozungumza Kirusi nchini Ukraine.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov, amebainisha kuwa, mwito wa kusitisha mapigano nchini Ukraine kwa sasa unapingana na makubaliano yaliyofikiwa baina ya marais wa Russia na Marekani huko Alaska.
Kabla ya hapo pia, Rais Vladimir Putin wa Russia alikuwa ameishambulia vikali Ulaya katika matamshi yake ya jana Jumanne, akitangaza kuwa nchi yake iko tayari kupigana vita na nchi za Ulaya. Amezishutumu nchi hizo za Ulaya kwa kufanya njama za kuharibu makubaliano ya kusimamisha mapigano nchini Ukraine kwa lengo la kuishinda Russia kiistratijia.