Maduro aapa Venezuela haitakubali "amani ya utumwa" ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i133860-maduro_aapa_venezuela_haitakubali_amani_ya_utumwa_ya_marekani
Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, amesema Caracas haitainama mbele ya shinikizo la kijeshi na kisiasa kutoka Washington, akisisitiza taifa hilo linapinga aina yoyote ya amani ambayo ni sawa na "utumwa" kwa Marekani.
(last modified 2025-12-03T02:50:23+00:00 )
Dec 03, 2025 02:50 UTC
  • Nicolás Maduro
    Nicolás Maduro

Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, amesema Caracas haitainama mbele ya shinikizo la kijeshi na kisiasa kutoka Washington, akisisitiza taifa hilo linapinga aina yoyote ya amani ambayo ni sawa na "utumwa" kwa Marekani.

Akihutubia umati uliokuwa ukipeperusha bendera za Venezuela nje ya Ikulu ya Miraflores Jumatatu, Maduro alisisitiza kuwa nchi yake inataka amani, lakini ni amani yenye uhuru, usawa na heshima ya taifa.

Aliukemea vikali "ujeuri wa kibeberu wa Marekani," akitangaza: "Hatutaki amani ya utumwa, wala amani ya kikoloni! Hatukubali ukoloni kamwe!

Serikali ya Marekani imeongeza shinikizo kwa Venezuela kupitia uimarishaji wa nguvu za kijeshi katika eneo Karibiani, ikidai ni operesheni ya kupambana na biashara ya dawa za kulevya bila ushahidi wenye mashiko. Venezuela inasema hatua hizo, zinazoongozwa na Rais Donald Trump na utawala wake, zinalenga kuipindua serikali ya Maduro na kutwaa rasilimali kubwa za taifa hilo, hususan utajiri wa mafuta na dhahabu. Venezuela ina akiba kubwa zaidi ya petroli duniani.

Wachambuzi wanasema kiwango cha harakati za kijeshi za Marekani kinazidi sana mahitaji ya operesheni ya kupambana na dawa za kulevya, kwani Washington imetuma askari 15,000, meli za kubeba ndege, meli za kivita na vikosi vya ndege vya F-35 katika ukanda huo.

Tangu Septemba, Marekani imefanya angalau mashambulizi 21 dhidi ya meli zinazodaiwa kubeba dawa za kulevya katika Karibiani na Pasifiki, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 83.

Maduro pia alilaani kampeni ya Marekani ya "ugaidi wa kisaikolojia" akisema: "Tumestahimili wiki 22 za mashambulizi… Katika wiki hizi 22 wananchi wa Venezuela wameonesha mapenzi yao kwa taifa."

Mkutano huo wa Jumatatu uliambatana na taarifa kwamba Rais Trump alikutana na timu yake ya usalama wa taifa Ikulu ya White House kujadili "hatua zinazofuata" kuhusu Venezuela.