UNHCR: Watu 100,000 wamekimbia Kaskazini mwa Msumbiji huku machafuko yakishadidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133858-unhcr_watu_100_000_wamekimbia_kaskazini_mwa_msumbiji_huku_machafuko_yakishadidi
Watu takribani 100,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao kaskazini mwa Msumbiji ndani ya wiki mbili pekee. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Jumanne ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, ambalo limeonya juu ya mashambulizi kuongezeka na kuyakumba maeneo ambayo hapo awali yalikuwa salama, na hivyo kuongeza mzigo wa wahudumu wa kibinadamu waliokwisha elemewa.
(last modified 2025-12-03T02:48:30+00:00 )
Dec 03, 2025 02:48 UTC
  • Wakimbizi nchini Msumbiji
    Wakimbizi nchini Msumbiji

Watu takribani 100,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao kaskazini mwa Msumbiji ndani ya wiki mbili pekee. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Jumanne ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, ambalo limeonya juu ya mashambulizi kuongezeka na kuyakumba maeneo ambayo hapo awali yalikuwa salama, na hivyo kuongeza mzigo wa wahudumu wa kibinadamu waliokwisha elemewa.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Msumbiji, Xavier Creach amesema “Mgogoro huu unazidi kuzorota kwa kasi ya kutisha,” na kuongeza kuwa “Ghasia zinasambaa, familia zinakimbia kwa hofu, na uwezo wetu wa kukidhi mahitaji hauendani tena na kiwango cha mahitaji kilichopo.”

Watu walioweza kuingia maeneo salama wamesimulia mashambulizi ya usiku dhidi ya vijiji vyao, ambapo makundi yenye silaha yalichoma nyumba na kuwashambulia raia.

Mgogoro huu, ulioanza Cabo Delgado mwaka 2017, tayari umewafurusha watu zaidi ya milioni 1.3.

Lakini UNHCR inasema mwaka 2025 umeshuhudia mabadiliko ya hatari, huku mashambulizi yakitokea kwa wakati mmoja na kuenea hadi jimbo la Nampula eneo ambalo hapo awali lilikuwa kimbilio kwa maelfu ya wanaokimbia ghasia.

Kwa kukosa taarifa za mapema, familia zinafikia katika makazi ya muda Nampula yakiwemo shule, makanisa na maeneo ya wazi bila nyaraka, bila mahitaji ya msingi na bila usaidizi.

Creach amesema “Watu wanakimbia wakiwa wamebanwa na hofu kali, wakitembea kwa siku kadhaa bila chakula, maji au ulinzi. Wanawake na wasichana kwa namna ya pekee wako katika hatari kubwa ya manyanyaso na ukatili.”

UNHCR inatoa wito wa ufadhili wa haraka ili kuimarisha jitihada za kukabiliana na mgogoro, kusaidia jamii zinazowapokea wakimbizi na kuzuia hali isiwe mbaya zaidi.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Msumbiji ameongeza kuwa: “Wakati mahitaji yakiwa katika kiwango cha juu zaidi, sisi tunaishiwa rasilimali.” Aidha amesema “Ikiwa msaada hautapatikana sasa, hali itadorora kwa kasi.”

Shirika hilo linahitaji dola milioni 38.2 mwaka 2026 ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kaskazini mwa Msumbiji. Lakini ufadhili wa 2025 umesimama kwenye asilimia 50 tu ya dola milioni 42.7 zinazohitajika.

Creach ameonya kuwa “Bila ufadhili wa ziada, maelfu ya familia zitabaki katika hali ya sintofahamu”.