Wakuu wa ECOWAS wazuru Guinea-Bissau baada ya mapinduzi ya kijeshi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133854-wakuu_wa_ecowas_wazuru_guinea_bissau_baada_ya_mapinduzi_ya_kijeshi
Ujumbe wa upatanishi wa ngazi ya juu kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) ulifanya mkutano Jumatatu na viongozi wa mpito wa Guinea-Bissau kujadili njia ya amani ya kumaliza mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na mapinduzi ya kijeshi ya wiki iliyopita.
(last modified 2025-12-03T02:38:38+00:00 )
Dec 03, 2025 02:38 UTC
  • Wakuu wa ECOWAS wazuru Guinea-Bissau baada ya mapinduzi ya kijeshi

Ujumbe wa upatanishi wa ngazi ya juu kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) ulifanya mkutano Jumatatu na viongozi wa mpito wa Guinea-Bissau kujadili njia ya amani ya kumaliza mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na mapinduzi ya kijeshi ya wiki iliyopita.

Ujumbe huo ukiongozwa na Rais wa Sierra Leone na Mwenyekiti wa ECOWAS, Julius Maada Bio, ulikutana na viongozi wa mpito wakiongozwa na Rais wa Mpito Jenerali Horta Inta-A.

Baada ya kikao cha faragha, pande zote mbili ziliwaambia waandishi wa habari mjini Bissau kwamba walifanya “mazungumzo yenye manufaa.”

Bio alisisitiza msimamo wa jumuiya hiyo wa kulaani kuchukua madaraka kwa nguvu na kutaka kurejeshwa mara moja kwa utaratibu wa kikatiba pamoja na kuanzishwa tena kwa mchakato wa uchaguzi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Mpito wa Guinea-Bissau, Joao Bernardo Vieira, alisema mkutano huo ulikuwa “wenye tija kubwa.”

Alitangaza kuwa pendekezo la mpito wa mwaka mmoja litawasilishwa katika mkutano wa kilele wa ECOWAS uliopangwa kufanyika Desemba 14 mjini Abuja, Nigeria, ambapo ramani ya njia ya mpito itaamuliwa.

ECOWAS ilisitisha uanachama wa Guinea-Bissau katika vyombo vyake vya maamuzi Alhamisi iliyopita kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais Umaro Sissoco Embalo.

Wakati wa ziara yao mjini Bissau, wajumbe wa upatanishi walikutana pia na maafisa wa uchaguzi ili kubaini kama wangeweza kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais.

Hata hivyo, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika Magharibi na Sahel, Leonardo Simao, alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Guinea-Bissau imesema haina uwezo wa kuchapisha matokeo ya uchaguzi wa urais na bunge kwa sababu haijakusanya matokeo yote.

Ujumbe wa upatanishi utawasilisha ripoti kwa wakuu wa nchi ambao watafanya uamuzi.

Jumatano iliyopita, kupitia taarifa iliyotangazwa katika televisheni ya taifa, kundi la maafisa wa kijeshi waliotambulisha kama “Kamandi Kuu ya Kijeshi ya Urejeshaji wa Usalama wa Taifa na Utaratibu wa Umma” lilitangaza kuwa limechukua madaraka yote ya dola.

Mapinduzi hayo yalifanyika wakati mgombea huru Fernando Dias na kambi ya Rais Embalo walidai ushindi katika uchaguzi wa urais wa Novemba 23, huku taifa likisubiri matokeo rasmi.