UN yatahadharisha kuhusu janga la njaa linalotishia wakimbizi nchini Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133824-un_yatahadharisha_kuhusu_janga_la_njaa_linalotishia_wakimbizi_nchini_ethiopia
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP) limeonya kwamba wakimbizi nchini Ethiopia wako katika hatari ya kufa njaa kutokana na uhaba mkubwa wa fedha unaolilazimisha shirika hilo kupunguza mgao wa chakula.
(last modified 2025-12-02T02:42:28+00:00 )
Dec 02, 2025 02:42 UTC
  • UN yatahadharisha kuhusu janga la njaa linalotishia wakimbizi nchini Ethiopia

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP) limeonya kwamba wakimbizi nchini Ethiopia wako katika hatari ya kufa njaa kutokana na uhaba mkubwa wa fedha unaolilazimisha shirika hilo kupunguza mgao wa chakula.

WFP imeripoti kwamba imelazimika kupunguza mgao wa chakula mwezi Oktoba kwa wakimbizi 780,000 kutoka Sudan na Sudan Kusini katika kambi 27 katika maeneo mbalimbali ya Ethiopia kutoka 60% hadi 40% pekee, ikimaanisha kwamba kila mtu sasa atapokea msaada wa chakula sawa na chini ya kalori 1,000 kwa siku.

Mkurugenzi na mwakilishi wa Mpango wa Chakula Duniani nchini Ethiopia, Zlatan Milišić amesema: "Tunachukua maamuzi yasiyowezekana. Tunajaribu kuwafikia wakimbizi wengi kadiri iwezekanavyo kwa kiasi kinachofaa cha msaada wa chakula."

Milišić ameonya kuwa: "Bila ya kuwa na pesa zaidi, kupunguzwa huku kwa misaada ya chakula kutakuwa hatua nyingine ya kuelekea kwenye kusimamisha kabisa ugavi wa chakula, na kuhatarisha maisha ya wale tunaowasaidia kwa sasa.”

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, kila hatua ya kupunguzwa mgao wa chakula kwa wakimbizi walioko nchini Ethiopia ina maana ya kuwepo watoto zaidi wenye njaa, mama anayelazimika kuruka mlo, na familia nyingine inayoelekea kwenye ukingo wa njaa.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani limetoa wito wa dharura wa kutolewa dola milioni 230 kwa ajili ya kusaidia shughuli za kibinadamu katika kipindi cha miezi sita ijayo, likisisitiza kwamba bila ufadhili mpya wa haraka, mpango huo unaweza kulazimika kusimamisha kabisa msaada wa chakula kwa wakimbizi wote nchini Ethiopia katika miezi ijayo.