Burundi, UNHCR kuwarejesha makwao wakimbizi wa Kongo
Serikali ya Burundi, kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), imetangaza mpango wa kuwarejesha makwao kwa hiari maelfu ya wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaoishi nchini humo.
Mpango huo, unaotarajiwa kuanza kutekelezwa Alhamisi wiki hii, unaashiria hatua muhimu katika juhudi za kikanda za kupata suluhisho la kudumu kwa watu waliokimbia makazi yao kutokana na mazingira tete ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Taarifa ya pamoja ya serikali ya Burundi na UNHCR imeeleza kuwa kurejeshwa nchini wakimbizi hao wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni sehemu ya maamuzi ya hiari, kwa mujibu wa chaguo huru la kila mtu anayehusika.
Mwezi Februari mwaka huu Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa lilisema kuwa kambi ya Busuma inayohifadhi wakimbizi wa Kikongo wasiopungua 66,000 waliowasili Burundi tangu mwishoni mwa mwaka jana, ilikabiliwa na uhaba mkubwa wa maji safi, chakula, dawa, malazi na huduma za ulinzi.
Maafisa wa UNHCR wamesisitiza kuwa hakuna mtu atakayelazimishwa kurudi Kongo na imewataka wakimbizi wanaotamani kurejea nyumbani kuripoti katika vituo vilivyoandaliwa ili kukamilisha taratibu za kiutawala, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa kuwakutanisha na familia zao wakimbizi watakaorejea Kongo.