Kwa Nini Trump Ameikasirikia NATO?
Rais Donald Trump wa Marekani, kwa upande mmoja, analimezea mate eneo lote la ardhi ya Canada ambayo ni mwanachama wa NATO, na kwa upande mwingine, ameonyesha kuwa, ana dhamira ya kuinyakua sehemu kubwa ya ardhi ya Denmark, ambayo nayo pia ni mwanachama wa shirika hilo la kijeshi.
Hasira za Trump dhidi ya shirika kuu la kijeshi la nchi za Magharibi zinazidi kushtadi siku baada ya siku. Katika siku za karibuni, rais huyo wa Marekani aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social: "NATO haikutusaidia huko nyuma na wala haitatusaidia katika siku za usoni."
Maelezo hayo ya Trump yanaashiria msimamo wa shirika la kijeshi la NATO wa kukataa kujiunga na Washington katika vita vya kichokozi ilivyoanzisha Marekani kwa kushirikiana na Israel dhidi ya Iran. Wakati wa mashambulio ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yaliyoanza tarehe 28 Februari mwaka huu na kuendelea kwa muda wa takriban siku 40, nchi wanachama wa NATO zilikataa kujiingiza katika vita hivyo. Baadhi ya viongozi wa nchi wanachama wa NATO walitamka kinagaubaga kuwa vita hivyo si vita vinavyoihusu NATO na hakuna sababu yoyote ya kuishambulia kijeshi Iran.
Kwa mujibu wa mkataba wa NATO, endapo nchi moja mwanachama wa shirika hilo itashambuliwa, nchi zingine zote wanachama zitakuwa na wajibu wa kujiunga na vita ili kumhami mwanachama mwenzao, ukiwa ni msingi wa kujihami kwa pamoja. Kwa kuzingatia kuwa Iran haikuwa imeishambulia kijeshi Marekani mnamo Februari 28, kanuni ya kujihami kwa pamoja haikupata msingi wa kisheria wa kutumiwa na nchi wanachama wa NATO. Muelekeo huo uliofuatwa na shirika hilo la kijeshi la Magharibi umemhamakisha na kumkasirisha sana rais wa Marekani, ambaye nchi yake ndiye mwanachama mkuu. Katika wiki za hivi karibuni, Trump amerudia mara kadhaa matamshi makali na ya kejeli dhidi ya NATO na nchi zake wanachama ikiwa ni pamoja na kuliita shirika hilo la kijeshi la Magharibi ‘chui wa karatasi’.
Lakini mbali na hayo, Trump amewahi mara moja kutamka hadharani kwamba anafikiria kuiondoa Marekani katika NATO, hatua ambayo kama itachukuliwa, itapelekea kusambaratika taasisi hiyo kuu ya kiusalama ya nchi za Magharibi. Hii ni pamoja na kuwa, bunge la Marekani tayari limeshapitisha sheria inayosisitiza kuwa kujiondoa Marekani katika NATO kutawezekana tu kufanywa kwa idhini ya bunge hilo, na haionekani kama uamuzi huo uliotangazwa na Trump utaweza kupata uungaji mkono wa Kongresi.
Pamoja na hayo, inavyoonekana, Trump anakusudia kuendeleza vita vyake vya maneno dhidi ya NATO pamoja na vitisho vya kujiondoa katika shirika hilo la kijeshi, huku akiendelea kuzibana nchi wanachama zikubali kutekeleza ajenda ya kushupalia vita inayofuatiliwa na Marekani katika kila pembe ya dunia, kuanzia Ukraine na Venezuela hadi Iran na China.
Wakati huohuo, mielekeo ya rais wa sasa wa Marekani ya kutumia mabavu na vitisho dhidi ya NATO imezusha hofu na wasiwasi mkubwa miongoni mwa washirika wa kijeshi wa Marekani katika pande mbili za Atlantiki.
Bila kujali wala kuzingatia maoni ya nchi zingine wanachama wa NATO kuhusu vita vya Ukraine, Trump ameishinikiza Kiev ikubali kutoa sehemu ya ardhi ya nchi hiyo kwa ajili ya kumaliza vita na Russia; hatua ambayo imewatia hofu washirika wa Marekani wa barani Ulaya.
Lakini mbali na hayo, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, utawala wa sasa wa Marekani unaoongozwa na Donald Trump, umekuwa ukiingilia masuala ya ndani ya nchi wanachama wa NATO kwa namna inayolenga kuhakikisha vyama vya kihafidhina na wanasiasa wa nchi hizo wanaomshabikia Trump wanaingia madarakani.
Katika anga kama hiyo iliyotanda hofu na shaka kubwa ya wanachama wa NATO kwa Marekani ya Trump, rais huyo wa Marekani anaendelea kulalama na kuhoji, kwa nini taasisi hiyo ya kijeshi haiungi mkono sera za Washington. Hii ni katika hali ambayo hatima ya kuridhia matakwa ya Trump ni kuishia kukanyagwa maslahi ya kitaifa ya nchi hizo wanachama wa NATO na kuzifanya ziwe nyenzo tu za kutumiwa na rais huyo mbinafsi wa Marekani. Kuonyesha ungangari wa kupinga matakwa hayo kumemkasirisha sana Trump na kuhatarisha umoja na mshikamano wa ndani ya shirika hilo la kijeshi kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa…/