Kiongozi Muadhamu awashukuru Maulamaa wa Kisunni wa Hormozgan
-
Leader of the Islamic Revolution Ayatollah Seyyed Mojtaba Khamenei
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Hosseini Khamenei, ameelezea shukrani zake za dhati kwa wanazuoni na maulamaa wa Kisunni katika mkoa wa kusini mwa Iran wa Hormozgan, akisifu mshikamano wao na tamko lao la kutoa Bay’a yaani kiapo cha utii.
Ujumbe huo uliwasilishwa kwa maandishi kwa Maulamaa wa Kisunni na pia kwa wanafunzi wa vyuo vya Kisunni mkoani humo. Kiongozi Muadhamu amewashukuru kwa “kuonyesha huruma, ushirikiano, na tamko la kutoa Bay’a.”
Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu katika mkoa wa Hormozgan na Imamu wa Sala ya Ijumaa mjini Bandar Abbas, Sheikh Mohammad Ebadizadeh, alithibitisha kupokelewa kwa ujumbe huo, akisisitiza “hadhi ya juu ya umoja ndani ya Umma wa Kiislamu.”
Alisema kuwa ujumbe huo una “thamani kubwa” na ulitolewa kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa kitaifa, kukuza umoja, na kuimarisha mafungamano kati ya matabaka mbalimbali ya jamii ya Kiislamu.
Hali kadhalika, Sheikh Ebadizadeh alirejea kauli za wanazuoni wa Kisunni mkoani humo waliolaani mashambulizi ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani, yaliyopelekea kuuawa shahidi kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, pamoja na makamanda waandamizi wa kijeshi.
Amebainisha kuwa tamko lao la kutoa Bay’a kwa mrithi wake, Ayatullah Sayyid Mojtaba Hosseini Khamenei, linaonyesha “uamsho, uaminifu, na kujitolea kwao kwa misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu.”
Aliongeza kuwa majibu ya maandishi ya Kiongozi Muadhamu yanasisitiza nafasi muhimu ya wanazuoni wa Kiislamu katika kuendeleza heshima, nguvu, na malengo ya taifa.
Katika ujumbe wake, Ayatullah Khamenei aliwashukuru wanazuoni wa Kisunni wa mkoa huo kwa salamu zao za rambirambi na masikitiko yao kufuatia kuuawa shahidi Imam Khamenei.
Ayatullah Khamenei amesema: “Ningependa kutoa shukrani zangu kwa maneno yenu ya dhati kufuatia hatua hii.”
Imam Khamenei aliuawa shahidi katika mashambulizi ya anga ya Marekani na utawala wa Kizayuni mnamo Februari 28 sawa na tarehe 10 Ramadhani wakati tawala hizo mbili zilipoanzisha vita vya uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.