Umoja wa Mataifa wakosoa vitisho vipya vya Trump dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137878-umoja_wa_mataifa_wakosoa_vitisho_vipya_vya_trump_dhidi_ya_iran
Msemaji wa Umoja wa Mataifa amekosoa wazi vitisho vipya vya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu kushambulia miundombinu ya Iran endapo matakwa ya Washington hayatatekelezwa.
(last modified 2026-04-21T09:28:06+00:00 )
Apr 21, 2026 09:11 UTC
  • Umoja wa Mataifa wakosoa vitisho vipya vya Trump dhidi ya Iran

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amekosoa wazi vitisho vipya vya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu kushambulia miundombinu ya Iran endapo matakwa ya Washington hayatatekelezwa.

Amesema hakuna sababu yoyote inayoweza kuhalalisha uharibifu wa miundombinu ya taifa lolote au kusababisha maumivu na mateso kwa raia.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IRNA, Stéphane Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa, amewaambia wanahabari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuwa: “Ninarudia kile tulichokwishasema. Hakuna lengo la kijeshi linaloweza kuhalalisha uharibifu kamili wa miundombinu ya kiraia au kulenga kuwaletea raia mateso kwa makusudi.”

Kuhusu hali ya sasa katika Lango Bahari la Hormuz, Dujarric ameongeza kuwa: “Tumeshuhudia shughuli nyingi na, kusema ukweli, kuna hali ya mkanganyiko mkubwa kuhusu kile kinachoendelea katika eneo la Hormuz.”

Aidha amesema: “Kilicho wazi kwetu ni kwamba Katibu Mkuu bado ana wasiwasi mkubwa kuhusu vizuizi vinavyoendelea kutumika na matukio ya baharini tuliyoyaona ndani ya saa 48 zilizopita.”

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amebainisha: “Msimamo wetu uko wazi: ni lazima tuone urejeshaji kamili wa haki za kimataifa za usafirishaji majini na uhuru wa meli kupita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, na hili linapaswa kuheshimiwa na pande zote.”

Akizungumzia athari za vita vya Marekani dhidi ya Iran na hali ya Lango Bahari la Hormuz ameongeza kuwa: “Kama sikosei, takribani asilimia 10 hadi 12 ya mbolea inayotumiwa duniani imekwama. Tumeona ongezeko la bei ya mbolea na urea.”

Aidha, amesema bei ya mafuta “siyo tu imepanda, bali imepanda katika mazingira yasiyo na utulivu wowote.”

Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa masuala haya yote yanaathiri mashirika ya Umoja wa Mataifa, uwezo wao wa kupanga na kufanya ununuzi kwa ufanisi.

Ikumbukwe Marekani baada ya kuanzisha vita dhidi ya Iran na kukabiliwa na matokeo mabaya ya kiuchumi na kisiasa, sasa inajaribu kujinasua kutoka katika kinamasi kupitia kile inachokiita diplomasia ya “amani kwa njia ya nguvu.” Kwa upande mmoja inatuma ishara chanya na kudai kuwa iko tayari kwa mazungumzo, na kwa upande mwingine inaendelea kutumia vitisho na mashinikizo ili kufikia matakwa yake katika meza ya mazungumzo. Wakati ikizungumza juu ya majadiliano, Marekani bado inaendeleza mzingiro wa kijeshi baharini dhidi ya Iran katika kipindi cha kusitisha vita, jambo ambalo ni ukiukaji wa wazi wa mapatano hayo.