Kwa nini Marekani inafanya njama za kuidhibiti Venezuela?
Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesisitiza kuwa, nchi yake itaendelea kulinda rasilimali zake kwa nguvu zote mbele ya tamaa ya kuchupa mipaka ya Marekani.
Kwa mujibu wa Pars Today, Rais Nicolas Maduro amelaani vitendo vya Marekani dhidi ya Caracas na kuzitumia ujumbe nchi zenye utajiri wa mafuta akisema kwamba Venezuela itatetea rasilimali zake za nishati kwa nguvu zake zote. Katika ujumbe uliosomwa na naibu wake Delcy Rodriguez katika mkutano wa OPEC Plus kwa njia ya Intaneti, Maduro amesema kwamba lengo la njama za Marekani katika Bahari ya Karibi ni kudhibiti akiba kubwa ya mafuta ya Venezuela kupitia hatua kali za kijeshi dhidi ya eneo hilo na dhidi ya wananchi na taasisi za Venezuela, na kwamba Caracas itatetea rasilimali zake za nishati kwa ukakamavu wa hali ya juu na haitosalimu amri mbele ya vitisho na mashinikizo ya Marekani.
Kauli za Maduro zimetolewa huku Washington ikiwa imetuma meli za kivita, manowari, ndege za kijeshi na wanajeshi katika pwani ya Venezuela tangu mwezi Agosti kwa kisingizio cha kupambana na dawa za kulevya, na inaendelea kutumia kisingizio hicho ili kuhalalisha hatua za kijeshi za Trump kwenye eneo hilo. Hii ni katika hali ambayo kwenye siku za hivi karibuni jeshi linalodhibitiwa na Trump limekuwa likizungumzia uwezekano wa kufanya shambulio la kijeshi dhidi ya Venezuela na kuipindua serikali halali ya kitaifa inayoongozwa na Rais Maduro huko Venezuela.
Mashinikizo ya Trump kwa Venezuela yameongezeka huku nchi hiyo na nchi nyingine za Amerika ya Kusini zikiwa zinahesabiwa kwamba ni ngome ya Marekani kwa muda mrefu bali kwa karne nyingi. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, hasa kutokana na mabadiliko ya kisiasa na kimataifa katika ukanda huo na dunia kwa ujumla, nchi za Amerika ya Latini, hasa Venezuela, zimeamua kufuata njia mpya na kupitisha sera za kupinga ukoloni na kujikomboa kutoka kwenye makucha kandamizi ya Marekani.
Matukio hayo yamekuwa na hasara kubwa kwa Marekani ambayo haiwezi kuendesha mambo yake bila ya kupora utajiri wa mataifa mengine tena kwa miaka mingi. Ni kwa sababu hiyo ndio maana mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi ya Washington dhidi ya Venezuela yameongezeka kwa njia ya vikwazo vikali na kuyachochea na kuyasaidizi makundi ya upinzani wa ndani, kwa sababu Marekani haiwezi kukubali kuona kwamba nchi za ukanda wa Amerika ya Kusini zinatoka kwenye udhibiti wake.
Hivi sasa Marekani inahitajia mno rasilimali za nishati, na nchi kama Venezuela zina utajiri mkubwa wa nishati inayohitajiwa na Marekani. Lakini viongozi wa Venezuela wameamua utajiri wa nchi yao uwanufaishe wananchi na si madola ya kibeberu. Hivi sasa ikulu ya Marekani, White House chini ya udhibiti wa Donald Trump imeelekeza nguvu zake zote kwenye kuipindua serikali halali na ya kizalendo ya Venezuela na kuweka madarakani serikali bandia na kibaraka ambayo italinda maslahi yake haramu ya kukomba utajiri wa nchi hiyo. Venezuela ina utajiri wa zaidi ya mapipa bilioni 303 ya akiba ya mafuta iliyothibitishwa. Utajiri huo ni sawa na asilimia 21 ya akiba yote ya mafuta duniani.
Mbali na mafuta, Venezuela ina zaidi ya futi za ujazo trilioni 200 za akiba ya gesi asilia, ambayo inaifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi kumi zenye utajiri mkubwa zaidi wa gesi ulimwenguni. Utajiri huo mkubwa unaifanya Venezuela kuwa na nafasi muhimu sana katika soko la nishati duniani. Kama nchi hiyo itaweza kusimamia rasilimali zake bila ya kuitegemea Marekani na makampuni ya Magharibi, inaweza kubadilisha mlingano wa nguvu za nishati duniani, na hicho ndicho kitu ambacho Washington haitaki kukisikia kabisa.
Kwa kweli, Marekani inaziona rasilimali za nishati za Venezuela kama vile si utajiri wa wananchi wa Venezuela bali ni mali ya akina Trump na wenzake. Wakati huo huo, Venezuela, yenye akiba kubwa zaidi ya mafuta duniani, inahesabiwa kuwa ni tishio lisiloepukika kwa udhibiti wa nishati wa Marekani. Kwa hivyo, Washington inajaribu kudhibiti rasilimali hizo, ili iwe na nguvu kubwa na isiwe na mpinzani katika soko la mafuta duniani. Sasa kama Venezuela itaweza kushinda mashinikizo na kudumisha uhuru wake, itakuwa imetoa ujumbe wa matumaini si tu kwa wananchi wa nchi hiyo, bali pia kwa ukanda mzima wa Amerika ya Kusini; naam, matumaini ya ukombozi kutoka kwenye udhibiti wa karne nyingi wa Marekani.