Je dunia kweli imekubali uongozi wa Marekani?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i136626-je_dunia_kweli_imekubali_uongozi_wa_marekani
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amedai dunia imekaribisha nafasi ya uongozi wa Marekani.
(last modified 2026-02-14T10:42:01+00:00 )
Feb 14, 2026 10:42 UTC
  • Michael Waltz
    Michael Waltz

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amedai dunia imekaribisha nafasi ya uongozi wa Marekani.

Michael Waltz amedai kuwa aghalabu ya nchi duniani zimeunga mkono kurejea Marekani katika nafasi ya kuiongoza  dunia. 

Waltz ambaye alikuwa akihutubia Mkutano wa Usalama wa Munich ametetea hatua iliyozusha mjadala mkubwa ya Washington ya kumteka nyara na kumhamisha Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro hadi Marekani, na kusema kwamba kuchukua tena Marekani uongozi wa dunia kumeungwa mkono nyuma ya pazia na nchi kadhaa.  Waltz ameeleza kuwa hatua hiyo ni ishara  ya "uongozi wa Marekani" na kuongeza kuwa viongozi wa nchi za nje mara kadhaa wamepongeza hatua hiyo katika mazungumzo ya faragha. Walt amesema haya katika hali ambayo, uvamizi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Venezuela na kumteka nyara Maduro vimekosolewa pakubwa kote duniani. 

Waltz pia amedai kuhusu bajeti ya Umoja wa Mataifa kwamba Marekani inataka kurejea kwenye misingi ya awali ya taasisi hiyo kwa kujikita katika kuanzisha na kudumisha amani, na kwamba inataka kutimizwa majukumu ambayo hayajatekelezwa. 

Madai kwamba nchi za dunia zimekaribisha pakubwa uongozi wa Marekani duniani, kama ilivyoelezwa katika hotuba na balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa ni kinyume na ushahidi na hali halisi ya dunia ya leo, na vilevile mchakato wa kimuundo wa mfumo wa kimataifa. Uchunguzi wa nyendo za serikali, taasisi za kimataifa na fikra za umma katika maeneo mbalimbali duniani unaonyesha kuwa ingawa Marekani inajaribu kujidhihirisha kuwa bado ni mchezaji muhimu kimataifa, lakini "kukubali uongozi" kunatofautiana na "uvamizi na kutumia mabavu". 

Matukio ya kijiopoliti katika muongo mmoja wa karibuni yanaonyesha uwepo wa harakati ya mfumo wa kimataifa kuelekea ulimwengu wa kambi kadhaa. Madola makubwa na ya kati yanafanya kila yawezalo kuimarisha uhuru wao wa kimkakati. Hata Umoja wa Ulaya ambao ni muitifaki na mshirika wa jadi wa Washington hususan baada ya migogoro ya kiusalama kama vita vya Ukraine na mgogoro wa nishati, na pia mashinikizo endelevu ya Marekani  kwa ajili ya kubebe mzigo wake wa gharama za usalama, unazidi kutilia mkazo sana dhana ya "kujitegemea kimkakati." Ingawa mbinu hii haina maana ya kujiweka mbali kikamilifu na Washington, lakini inaonyesha kwamba hata washirika wa karibu sana wa Marekani pia hawataki kuarifishwa katika fremu ya  uongozi wa upande mmoja wa Marekani.

Sera ya mambo ya nje ya nchi nyingi zinazoinukia kiuchumi, hasa wanachama wa kundi la BRICS, imejikita katika uwepo wa mlingano kati ya nchi mbalimbali. Nchi kama India, Brazil na Afrika Kusini, katika miaka ya karibuni zimepanua uhusiano wao wa kiuchumi na kiusalama kwa wakati mmoja na Magharibi na Mashariki. Mienendo hii inaonyesha matakwa ya nchi hizo ya kuwepo mfumo wa kimataifa wa kambi kadhaa na usioegemea upande wowote; na si kuunga mkono mfumo wa upande mmoja chini ya uongozi wa Marekani. Kukuza ushirikiano wa Kusini-Kusini na kuimarisha makundi ya kimataifa kama vile BRICS pia kunadhihirisha mwelekeo huu. 

Kundi la BRICS 

Ushindani mkubwa wa kugombea madaraka bado ni kikwazo kikubwa kwa makubaliano ya kimataifa kuhusu uongozi wa Marekani. China inataka kupanua ushawishi wake wa kitaasisi na kifedha kupitia mipango ya kimataifa ya kiuchumi na miundombinu, na wakati huo huo inasisitiza kuzidisha  kasi ya uwezo wake wa kijeshi ili kujitayarisha kwa makabiliano yanayoweza kujiri kati yake na Marekani katika siku zijazo. Russia pia inataka kuimarisha nafasi yake katika milingano ya usalama, kwa uchache katika ngazi ya Ulaya kupitia njia ya kijeshi na sekta ya nishati. Uwepo hai wa wahusika hawa umekuwa sababu ya nchi nyingi kuwa na machaguo mbadala ya ushirikiano na kutokuwa utegemezi kwa Washington. 

HItilafu za kisiasa kati ya Marekani na waitifaki wake wa kijadi hasa Ulaya na hata hitilafu za nchi hiyo na Canada kuhusu masuala ya kibiashara, na madai ya Trump ya ulazima wa kujiunga nchi hiyo na Marekani, na pia mvutano kati ya Marekani na Denmark kuhusu madai ya Washington kuhusiana na kisiwa cha Greenland, vinabatlisha dhana potofu ya kukubalika uongozi wa Marekani duniani kote. Wakati huo huo, mivutano kati ya Marekani na waitifaki wake wa Magharibi kuhusu sera za kibiashara, vikwazo au mbinu za kusimamia migogoro ya kikanda inaonyesha kuwa uongozi wa Washington hauungwi mkono  hata katika kambi ya Magharibi kwenyewe.  

Fikra za umma duniani kuhusu uongozi wa Marekani, hasa katika duru ya pili ya urais wa Donald Trump ni hasi sana. Chunguzi za maoni kimataifa zilizofanywa katika miaka ya hivi karibuni zinaonyesha kuongezeka pakubwa hali ya kutokuwa na imani waliowengi kuhusu sera za uvamizi wa kijeshi, vikwazo na hatua za kindumakuwili za Washington. Hasa ikizingatiwa kuwa Trump anafanya kila awezalo kufanikisha malengo yake ya kujitanua kupitia mabavu katika kalibu ya sera ya amani kupitia nguvu na mabavu.

Hatimaye, inatupasa kuelewa kuwa dhana ya uongozi imebadilika katika karne ya 21. Aghalabu ya nchi zinataka  “uongozi wa mtandao” unaozingatia ushiriki wa pande zote, sheria za pamoja na kugawana majukumu, ilhali Marekani ya Trump inachukua hatua kinyume na mwenendo huu.