Amnesty yataka uchunguzi wa uhalifu wa kivita wa RSF nchini Sudan.
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133920-amnesty_yataka_uchunguzi_wa_uhalifu_wa_kivita_wa_rsf_nchini_sudan.
Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limetaka kufanyike uchunguzi wa uhalifu wa kivita kuhusu shambulio lililofanywa na kundi la waasi la Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Zamzam, jimbo la Darfur Kaskazini, mapema mwaka huu.
(last modified 2025-12-04T12:14:54+00:00 )
Dec 04, 2025 12:14 UTC
  • Amnesty yataka uchunguzi wa uhalifu wa kivita wa RSF nchini Sudan.

Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limetaka kufanyike uchunguzi wa uhalifu wa kivita kuhusu shambulio lililofanywa na kundi la waasi la Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Zamzam, jimbo la Darfur Kaskazini, mapema mwaka huu.

Ripoti iliyotolewa Jumatano inaeleza ukatili uliofanywa na waasi wa RSF wakati wa shambulio kubwa, ikiwemo mauaji holela na ubakaji wa halaiki. Mashambulio hayo yalifanyika kati ya Aprili 11 na 13, ambapo wapiganaji wa RSF walitumia vilipuzi katika maeneo yenye raia na kufyatua risasi kiholela katika makazi ya raia. Mashuhuda wamesema waliona angalau raia 47 wakiuawa wakiwa majumbani mwao, wakikimbia au wakijificha msikitini.

Katibu Mkuu wa Amnesty, Agnes Callamard, amesema: “Shambulio la kikatili na la makusudi dhidi ya raia wenye njaa katika kambi ya Zamzam limeonyesha tena dharau ya kutisha ya RSF kwa maisha ya binadamu.”

Ripoti hiyo pia imeikosoa tena Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kuunga mkono waasi wa RSF, ingawa UAE imekanusha taarifa kuwa inatoa silaha au msaada wa kifedha kwa waasi hao.

Kwa sasa waasi wa RSF wanadhibiti jimbo lote la Darfur Kaskazini na inasonga mashariki kuelekea Kordofan Magharibi, hali inayoongeza idadi ya watu waliolazimika kuhama. Tangu Aprili 2023, mapigano kati ya RSF na jeshi la Sudan (SAF) yamesababisha vifo vya makumi ya maelfu na kuwalazimisha takribani watu milioni 12 kuyahama makazi yao. Juhudi za kusaka maridhiano hadi sasa hazijafanikiwa.