Mapigano yashadidi DRC, kila upande unamtuhumu mwenzake
Mapigano yamezidi kupamba moto mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huku jeshi na waasi wa M23 kila upande ukimshutumu mwenzake kwa kukanyaga makubaliano ya kusitisha mapigano.
Katika taarifa yake, Sylvain Ekenge, msemaji wa Jeshi la DRC (FARDC), amelaani mlolongo wa mashambulizi ya waasi wa M23 kwenye maeneo ya jeshi la Congo katika Mkoa wa Kivu Kusini, ambapo maeneo kadhaa, ikiwa ni pamoja na Bukavu, makao makuu ya mkoa huo, yametekwa na waasi.
Kwa upande wao, waasi wa M23, wameituhumu serikali ya Kinshasa kuwa ndiyo iliyoanzisha mashambulizi makubwa katika maeneo yenye watu wengi pamoja na katika safu zote za mbele huko Kivu Kusini. Msemaji wa M23 Lawrence Kanyuka amedai kwamba vikosi vya FARDC vimeshambulia mji wenye watu wengi wa Kamanyola ulioko kwenye njia panda ya kimkakati ambayo sasa inashikiliwa na waasi; na kuua kwa uchache raia watatu na kuwajeruhi wengine watano. Kwa mujibu wa duru za Umoja wa Mataifa, mapigano makali na ya pande nyingi yalitokea jana Jumanne huko Kivu Kusini na kuongeza hofu kwa raia waliokwama katikati ya pande zinazopigana.
Mapigano yameongezeka hivi sasa licha ya kuweko makubaliano ya kusitisha vita kati ya jeshi la DRC na waasi M23. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, inabidi kila upande uchukue hatua za kujenga imani kuelekea kwenye kusitisha mapigano kikamilifu.
Kesho Alkhamisi, Rais Felix Tshisekedi wa DRC na Rais mwezake wa Rwanda, Paul Kagame wanatarajiwa kukutana nchini Marekani kwa ajili kuidhinisha makubaliano ya amani ambayo yalitiwa saini mwezi Juni na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili.