Meya wa Minneapolis apinga matamshi ya Donald Trump dhidi ya Wasomali
https://parstoday.ir/sw/news/world-i133902-meya_wa_minneapolis_apinga_matamshi_ya_donald_trump_dhidi_ya_wasomali
Maafisa katika mji wa Minneapolis nchini Marekani wameungana ili kuondoa hofu iliyotanda miongoni mwa jamii kubwa ya Wasomali katika mji huo.
(last modified 2025-12-04T10:49:36+00:00 )
Dec 04, 2025 07:45 UTC
  • Meya wa Minneapolis
    Meya wa Minneapolis

Maafisa katika mji wa Minneapolis nchini Marekani wameungana ili kuondoa hofu iliyotanda miongoni mwa jamii kubwa ya Wasomali katika mji huo.

Maafisa hao wamechukua hatua hiyo baada ya Rais Donald Trump kuzidisha mashambulizi yake dhidi ya wahamiaji wa Wasomali akisema wanapaswa kurejea walikotoka.

Meya, mkuu wa polisi na maafisa wengine wa mji wa Minneapolis wameungana ili kuondoa hofu katika jamii kubwa ya Wasomali wa mji huo huku kukiwa na ripoti kwamba mamlaka ya shirikisho inatayarisha operesheni iliyokusudiwa kuwalenga wahamiaji wa Kisomali katika jimbo la Minnesota.

Jacob Frey Meya wa mji wa Minneapolis kutoka chama cha Democrat amesema kuwa wanaipenda jamii ya Wasomali na wako bega kwa bega na jamii hiyo. Minneapolis inajivunia kuwa makazi ya jamii kubwa ya Wasomali katika nchi nzima.

"Wasomali wamekuwa wakiiishi Marekani kwa miongo kadhaa na kunufaika na "utamaduni na uthabiti wa kiuchumi wa jiji letu" , amesema Meya Jacob Frey.

Wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri uliofanyika jana Jumanne, Trump alianza tena kutoa kauli ya kibaguzi, akimwelezea Ilhan Omar na wahamiaji wengine Wasomali kuwa ni "takataka" tu na kuwataka waondoke Marekani.

"Tunaelekea kwenye njia isiyo sahihi kama tunaendelea kuingiza takataka nchini mwetu. Ilhan Omar ni takataka. Yeye ni takataka. Marafiki zake ni takataka," alitamka bila ya aibu rais huyo wa Marekani.

Trump ametoa tuhuma hizo dhidi ya jamii ya wahamiaji wa Kisomali katika hali ambayo, ripoti ya Chama cha Biashara cha Minnesota ya mwaka 2021 ilieleza kwamba, "japokuwa wakimbizi wengi Wasomali walifika huko wakiwa na elimu ndogo, viwango vya chini vya ushiriki wa wafanyakazi na viwango vya juu vya umaskini, hali yao miongo miwili baadaye imebadilika sana".