Uchaguzi Uganda: UN yalaani ukandamizaji dhidi ya mgombea urais wa upinzani
-
Uchaguzi Uganda: UN yalaani ukandamizaji dhidi ya mgombea urais wa upinzani
Umoja wa Mataifa jana Jumatano ulikosoa kuongezeka ukandamizaji dhidi ya upinzani na vyombo vya habari nchini Uganda kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi ujao, na kutaka uchunguzi ufanyike bila upendeleo kuhusu madai ya kukamatwa raia kiholela, kutoweka na "mateso".
Ofisi ya Haki ya Umoja wa Mataifa imeangazia "ripoti za kuaminika" zinazoonyesha kuwa takriban watu 550, wakiwemo wanachama na wafuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini Uganda cha National Unity Platform (NUP) na mgombea urais wa chama hicho Robert Kyagulanyi Ssentamu (Bobi Wine), walikamatwa na kuzuiliwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Watu zaidi ya 300 kati ya idadi hiyo tajwa walitiwa nguvuni tangu kuanza kampeni za uchaguzi mwezi Septemba mwaka huu kabla ya uchaguzi mkuu wa Januari 15 ambapo Rais wa sasa wa Uganda Yoweri Museveni anawania kusalia mamlakani. Museveni amekuwa mamlakani tangu mwaka 1986.
Taarifa ya Ofisi ya Haki ya Umoja wa Mataifa imebainisha kuwa aghalabu ya watu waliokamatwa wako kizuizini wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali kuanzia kutatiza umma na kero za umma na kutotii amri halali za kufanya mashambulizi, kuchochea ghasia n.k.
Ofisi ya Haki ya Umoja wa Mataifa pia imegusia namna askari usalama wa Uganda waliojizatiti pakubwa kwa silaha walivyosambazwa katika maeneo ambayo chama cha upinzani cha NUP kilipanga kufanya mikutano yake ya kampeni.
Taarifa ya ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema: askari usalama wa Uganda pia wametumia mabomu ya machozi, mijeledi, marungu, maji ya kuwasha na viuwasho vya kemikali miongoni mwa silaha nyingine wakati wa mikutano ya hadhara lengo likiwa ni kuwatawanya wafuasi wa chama cha upinzani cha NUP na hivyo kujeruhi watu wengi.