UN yalaani mashambulizi ya RSF huko Sudan, yataka vita vikomeshwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i137028-un_yalaani_mashambulizi_ya_rsf_huko_sudan_yataka_vita_vikomeshwe
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) limeelezea "wasiwasi mkubwa" kuhusu kuongezeka kwa ghasia na machafuko katika nchi iliyoathiriwa ba vita ya Sudan, hasa katika majimbo ya Darfur na Kordofan, likitaka mapigano yasitishwe mara moja.
(last modified 2026-02-25T09:23:00+00:00 )
Feb 25, 2026 09:23 UTC
  • Wakimbizi wa Sudan
    Wakimbizi wa Sudan

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) limeelezea "wasiwasi mkubwa" kuhusu kuongezeka kwa ghasia na machafuko katika nchi iliyoathiriwa ba vita ya Sudan, hasa katika majimbo ya Darfur na Kordofan, likitaka mapigano yasitishwe mara moja.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumanne, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililaani mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani dhidi ya wananchi wa kawaida, vituo vya kiraia na wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na "mashambulizi mengi yanayoathiri" Shirika la Chakula Duniani (WFP).

Wapiganaji wa kundi la waasi la Rapid Support Forces (RSF), wamelaumiwa kwa ongezeko la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya raia.

Maelfu ya watu wameuawa, na mamilioni wamelazimika kuhama makazi yao katika vita vya ndani vya Sudan ambavyo vimesababisha kile Umoja wa Mataifa unakielezea kama mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi na njaa duniani.

Mapema wiki hii, RSF ilifanya mashambulizi makubwa huko Misteriha katika Jimbo la Darfur Kaskazini, na kuua watu wasiopungua 28 na kujeruhi wengine 39, wakiwemo wanawake 10. Taarifa hiyo imetolewa na Mtandao wa Madaktari wa Sudan, ambao unafuatilia vita vinavyoendelea kwa kipindi cha miaka mitatu sasa nchini humo.

Baraza hilo pia limelaani "kuendelea kwa mashambulizi na uvunjifu wa amani katika eneo la Kordofan".

Taarifa ya Baraza la Usalama pia imelaani vikali aina zote za ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji unaofanywa dhidi ya raia.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la UN wamelaani ripoti za watu kuwekwa kizuizini kiholela na unyanyasaji wa kingono unaohusiana na kusisitiza kwamba vitendo hivyo vinaweza kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.