Uchaguzi Uganda; Bobi Wine apinga ushindi wa Museveni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135628-uchaguzi_uganda_bobi_wine_apinga_ushindi_wa_museveni
Kiongozi wa upinzani na mshindani mkuu wa Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi mkuu wa hivi karibuni nchini Uganda, Robert Kyangulani maarufu kama Bobi Wine amesema hakubaliani na matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo.
(last modified 2026-01-18T10:26:45+00:00 )
Jan 18, 2026 10:26 UTC
  • Uchaguzi Uganda; Bobi Wine apinga ushindi wa Museveni

Kiongozi wa upinzani na mshindani mkuu wa Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi mkuu wa hivi karibuni nchini Uganda, Robert Kyangulani maarufu kama Bobi Wine amesema hakubaliani na matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo.

Mwanasiasa huyo chipukizi anayekubalika na tabaka la vijana ametangaza kuwa hatambui rasmi matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika siku chache zilizopita. 

Ametoa wito kwa wafuasi wake kupinga matokeo hayo, akisema kizuizi cha mtandao kilitumika kuzuia ufuatiliaji wa makosa ya uchaguzi.

Bobi Wine amesema Museveni amefanya mambo mengi yanayoidhoofisha Uganda na kusisitiza kuwa hatoruhusu kuendelea kudhoofishwa kwa demokrasia ya nchi hiyo. 

Tume ya uchaguzi nchini Uganda imemtangaza Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Alkhamisi wiki hii, akiwa na jumla ya kura 7,946,772 ambayo ni asilimia 71.65% ya kura zote zilozopigwa.

Kwa mujibu wa tume hiyo, kura 11,366,201 zilipigwa katika uchaguzi huu wa mwaka 2026, ikiashiria asilimia 52.50% ya idadi ya wapiga kura waliojitokeza kushiriki.

Wachambuzi wa kisiasa wamesema matamshi ya Wine yanaweza kuzibadilisha siku zijazo huko Uganda kuwa za mchafukoge na mgogoro, na kuanza mzozo wa kuwania madaraka na kupigania demokrasia nchini humo. 

Wakati huo huo, serikali ya Uganda imetangaza kurejesha huduma za intaneti leo Jumapili baada ya kufungwa kwa siku tano nchini kote wakati wa uchaguzi mkuu, hatua ambayo mamlaka ilisema ililenga kupunguza matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.