Iran yaiambia Marekani: Vikwazo na vita vimefeli; jaribu diplomasia na kuheshimiana
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136986-iran_yaiambia_marekani_vikwazo_na_vita_vimefeli_jaribu_diplomasia_na_kuheshimiana
Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Iran amesema kuwa wakati umefika kwa Marekani kuachana na vikwazo vyake "visivyo na matunda" na sera iliyofeli ya vita dhidi ya Iran, akitilia mkazo kuheshimiwa kikamilifu diplomasia kama njia pekee ya kupiga hatua.
(last modified 2026-02-25T07:04:48+00:00 )
Feb 24, 2026 08:02 UTC
  • Kazem Gharibabadi
    Kazem Gharibabadi

Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Iran amesema kuwa wakati umefika kwa Marekani kuachana na vikwazo vyake "visivyo na matunda" na sera iliyofeli ya vita dhidi ya Iran, akitilia mkazo kuheshimiwa kikamilifu diplomasia kama njia pekee ya kupiga hatua.

Kazem Gharibabadi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayehusika na Masuala ya Kisheria na Kimataifa amesema katika hotuba yake jana mjini Geneva Uswisi katiak kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwamba maadui wa Iran wanaweza kuanzisha vita lakini hawawezi kuamua mwisho wake.

"Maadui wa Iran wamejaribu vikwazo na vita dhidi ya Iran na hawajafika popote. Umefika wakati sasa wa kupata tajiriba ya diplomasia na kuheshimiana," amesema Gharibabadi.

Ameongeza kuwa wananchi wa Iran hawana lengo la kuanzisha vita dhidi ya nchi nyingine zozote lakini watasimama imara dhidi ya uvamizi wowote wa kijeshi au chokochoko za kisiasa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na wataihami nchi yao. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayehusika na Masuala ya Kisheria na Kimataifa amebainisha kuwa matokeo ya vita hayataishia tu kwa wahusika kwenye mzozo, "lakini yataliathiri eneo zima.

Kwa upande wake, Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa haitaanzisha vita, lakini itajibu kwa nguvu hujuma yoyote ya kijeshi inayolenga mamlaka na usalama wake. Tehran imekumbusha kuwa mashambulizi ya Israel Marekani mwezi Juni mwaka jana yalisababisha Iran kujibu kwa makombora ya balistiki dhidi ya ngome za utawala wa Israel na kituo cha anga cha Al Udeid nchini Qatar, ambacho ni ngome muhimu zaidi ya kijeshi ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi.