UN yatahadharisha kuhusu vifo vinavyosababishwa na mabomu ya kutegwa ardhini
-
UN: Mabomu ya kutegwa ardhi ni hatari kwa maisha ya watu
Umoja wa Mataifa umetoa tahadhari kuhusu ongezeko la vifo vinavyosababishwa na mabomu ya kutegwa ardhini huku kukiwa na upungufu wa ufadhili wa programu za kutegua mabomu hayo.
Wataalamu wa kimataifa wanaokutana mjini Geneva wanasema urithi huo wa migogoro ya zamani na mipya unaendelea kuua na kulemaza raia karibu kila siku.
Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kutegua Mabomu (UNMAS) umesema kwamba ingawa kazi ya kutegua mabomu katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu na Sudan kwa sasa inafadhiliwa vya kutosha, lakini hali ilikuwa mbaya katika nchi za Afghanistan na Nigeria.
Mwakilishi wa UNMAS huko Geneva, Christelle Loupforest, amesema programu ya shirika hilo katika nchi hizo mbili na Ethiopia zinaweza kufungwa ifikapo Machi mwakani kama hakutapatikana msaada mpya wa wafadhili.
Nchini Sudan, hali bado ni ya kutisha sana kwa timu za kutegua mabomu yaliyotegwa ardhini ambazo zinahofia maisha ya raia milioni 1.5 ambao wamerudi Khartoum.
Mji huo mkuu wa Sudan ulikuwa kitovu cha awali cha mzozo unaoendelea kati ya vikosi vya Jeshi la Sudan na waasi wa Rapid Support Forces (RSF).
"Ni timu tano tu za UNMAS zinazofanya kazi nchini Sudan kwa sasa na "zote ziko Khartoum, kwa sababu mahitaji ni makubwa sana huko" amesema mkuu wa UNMAS nchini Sudan, Sediq Rashid.
Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa una wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya mji wa al-Fasher ambao ulizingirwa na waasi kwa zaidi ya siku 500.
Nchini Nigeria, timu za kutegua mabomu zina wasiwasi kwamba kutokana na kambi za jamii zilizopoteza makazi kufungwa, watu wanahatarisha maisha yao kwa kurudi katika maeneo yenye silaha hatari ambazo hazijalipuka.
Wataalamu wanaokutana Geneva wamesisitiza kwamba programu za kutegua mabomu ya ardhini, ambazo mara nyingi huonekana kama mipango ya muda mrefu ya uokoaji, kwa hakika ni hatua za dharura za kibinadamu zinazookoa maisha.