Wakimbizi wa Burundi watakiwa kuondoka Tanzania
-
Wakimbizi wa Burundi watakiwa kuondoka Tanzania
Serikali ya Tanzania imetangaza rasmi kufuta hadhi ya ukimbizi na kuzifunga kambi za wakimbizi wa Burundi waishio mkoani kigoma kabla ya mwezi Juni mwaka ujao wa 2026.
Uamuzi huo umetangazwa kwa nyakati tofauti na mamlaka za serikali ya Tanzania kupitia idara ya wakimbizi ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi na kuungwa mkoani na serikali ya Burundi ikisisitizwa kuwa wakimbizi wa Burundi hawana sababu za kuendelea kuishi uhamishoni wakati nchi yao ina amani
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania George Simbachawene ni miongoni mwa waliosisitiza msimamo huo wakati akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya Tanzania, Burundi na shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi, UNHCR.
Hivi karibuni viongozi wa Tanzania, serikali ya Burundi na UNHCR walizuru kambi za wakimbizi wa Burundi za Nduta wilayani Kibondo na Nyarugusu wilayani Kasulu na kuzungumza na maelfu ya wakimbizi, wakitangaziwa azimio la kufuta hadhi yao ya ukimbizi na kuhimizwa kurejea haraka nchini mwao.
Azimio la kufuta hadhi ya ukimbizi kwa Warundi linagusa mioyo ya wengi hasa waliozaliwa ukimbizini au waliopoteza wazazi ambao hawafahamu kwa kina asili yao.
Mwenyekiti wa kamati ya usalama mkoa wa Kigoma Inspekta Jenerali mstaafu wa jeshi la polisi Simon Sirro ambaye pia ni mkuu wa mkoa huo hashtushwi na mashaka ya wakimbizi na anasisitiza waache fikra za utegemezi na warejee nchini mwao kujenga taifa lao.
Balozi mdogo wa Burundi mkoani Kigoma Jeremie Kekenwa amesema kuwa azimio la kuhakikisha wakimbizi wa nchi yake wanarejea ni sahihi kwa kuwa Burundi ni nchi yenye amani na usalama wa kutosha
Tanzania inawahifadhi jumla ya wakimbizi 238,956, wakiwemo Warundi 152,019 na Wakongo 86,256 na wengine 681 kutoka mataifa mengine.