Mataifa ya Ulaya yakabiliwa na wimbi la joto kali
-
Mataifa ya Ulaya yakabiliwa na wimbi la joto kali
Mataifa ya Ulaya yanakabiliwa na wimbi la joto kali huku yakilazimika kuchukua hatua kadhaa ili kuepusha maafa.
Serikali ya Ufaransa imeviweka vikosi vya dharura na jeshi katika hali ya tahadhari kutokana na hatari ya kuzuka moto wa nyika huku ikipiga marufuku unywaji wa pombe hadharani.
Mataifa ya Ufaransa, Ujerumani na Uhispania yametangaza kufuta baadhi ya michezo iliyotarajiwa kufanyika nje, kutokana na wimbi kali la joto linaloyakumba mataifa mengi ya Ulaya, ambako katika baadhi ya maeneo kunatarajiwa hadi nyuzi joto zaidi ya 40 Celsius.
Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema zaidi ya watu 200,000 barani Ulaya wamefariki dunia kutokana na athari zinazohusiana na joto kali katika kipindi cha miaka minne iliyopita, huku vifo vingi vikielezwa kuwa vingeepukika.
Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa, vifo vinavyotokana na joto kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 65 viliongezeka kwa takriban asilimia 85 katika miongo miwili iliyopita, wakati asilimia 25 ya watoto wote hivi leo wanakabiliwa na joto la mara kwa mara na ifikapo 2050, idadi hiyo ianaweza kuongezeka hadi karibu asilimia 100.