Ramadhani, Mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu (5)
Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran na karibuni kusikiliza sehemu ya tano ya kipindi hiki maalumu tulichokutayarishieni kwa mnasaba wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhni.
Mwezi huu kama tunavyojua sote ni mwezi wa machipuo ya ibada, mwezi ambao milango ya rehema ya Mwenyezi Mungu hufunguliwa kwa ajili ya waja wake na ni mwezi ambao pia huambatana na fursa chungu nzima zisizo na mfano wake ambazo hutuandalia uwanja wa kujirudi na kurejea kwenye hakika ya maumbile yetu.
Jiungeni nasi katika anga na siku hizi za kimaanawi ili tupate kunufaika sote na baraka pamoja na fadhila kubwa za mwezi huu uliojaa nuru kupitia dua na ibada tunazofanya katika dhifa hii adhimu ya Mwenyezi Mungu. Mwezi wa Ramadhani ni fursa ambayo tunaweza kunufaika nayo kwa ajili ya kuhuisha nyoyo ili kumkurubia zaidi Mola wetu.
*******
Imam Khomeini (MA) mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran anasema: "Dhifa ya Mwenyezi Mungu ni hayo hayo madini ya adhama na nuru. Mwenyezi Mungu amewaalika waja wake kwenye karamu hii lakini kama mja mwenyewe hafai, hawezi kunufaika na hadhi kubwa na ya fahari kama hii."
Ramadhani ni dhifa hii ya Mwenyezi Mungu ambayo inasubiri jibu letu. Mwenyezi Mungu Mtukufu ametualika kwenye karamu hii maalumu ambapo humo kuna kila aina ya baraka, raha na ladha za kiroho. Lakini sharti la kuingia na kunufaika na dhifa hii ni kujiweka tayari kiroho. Nyoyo chafu na zilizojaa maovu haziwezi kunufaika na ladha za kimaanai na hakika za kiroho zilizoko kwenye dhifa hii. Pazia za giza ambazo zimezifunika nyoyo zetu na hivyo kuzuia mawasiliano ya moja kwa moja na Mwenyezi Mungu zinapaswa kuondolewa ili kuziruhusu nyoyo zishiriki kwenye karamu hii iliyojaa nuru ya Mwenyezi Mungu.
Katika mwezi huu mtukufu, sisi hupewa fursa nyingine ya kuzitakasa nyoyo zetu kupitia usomaji Qur'ani, dua za alfajiri na usiku na kutubia dhambi zetu ili kuondoa kutu ya dhambi iliyoko nyoyoni na hivyo kufungua milango ya rehema kuelekea kwa Mwenyezi Mungu.
**********
Ili kuingia kwenye karamu hii adhimu na ya fahari kwa ajili ya kunufaika na baraka za funga, masuala matatu yanapasa kuzingatiwa, ambayo ni uelewa, hamu na adabu au desturi za funga. Hatua ya kwanza ni uelewa na ufahamu. Uelewa una maana kwamba iwapo mja atakuwa na mtazamo wa kiirifani na ufahamu wa kutosha kuhusiana na mwezi mtukufu wa Ramadhani bila shaka atanufaika zaidi na baraka za mwezi huu na hivyo kuathiri moyo wake. Kuhusiana na umuhimu wa uelewa, Mtukufu Mtume (saw) alimwambia Imam Ali (as): "Ewe Ali! Usingizi wa aalim ni bora kuliko ibada ya mtu jahili."
Uelewa na ufahamu bila shaka humuongezea mja hamu ya kuimarisha malengo yake ya kimaanawi. Kati ya mafundisho yake, Qur'ani Tukufu inalipa umuhimu mkubwa suala la kutafakari na kuwasifu watu ambao hutukuza na kumtaja Mwenyezi Mungu huku wakiwa wanatafakari kuhusu maajabu ya uumbaji wa mbingu na ardhi. Umuhimu huu unaotolewa na Qur'ani Tukufu na vile vile mafundisho ya Ahlul Bait wa Mtume (saw) kuhusu suala zima la kutafakari unatokana na ukweli kwamba kutafakari huondoa pazia za kughafilika na kumuwezesha mwanadamu kufikia haki na hakika mpya. Ni sawa kabisa na anavyosema Allama Tabatabai, mfasiri mkubwa wa Qur'ani Tukufu kuwa: "Kila mara ninapotalii Qur'ani, mimi hupata kujua mambo mapya na Qur'ani huniambia maneno mapya."
*********
Jambo jingine ambalo lina umuhimu mkubwa katika mwezi huu wa Ramadhani ni kuwa na hamu na shauku ya kufanya ibada. Juhudi za kiroho na hisia anazokuwa nazo mja kuhusu funga ya mwezi wa Ramadhani humfanya adiriki vyema thamani ya ibada hii. Watu wenye imani hupenda funga kwa sababu Mwenyezi Mungu amesisitiza juu ya utekelezaji wake. Kwao funga ni mazoezi ya kijitolea, kujinyima na kuvumilia magumu. Katika mwezi huu, mwanadamu kupitia funga anaweza kupunguza matamanio yake ya kimwili na kujiweka mbali na mafungamano ya kidunia na hivyo kuwa mwepesi katika harakati yake ya kumkurubia Muumba wake.
Mtume Mtukufu (saw) anasema: "Mbora wa watu ni yu anayeashiki ibada. Hivyo huikumbatia ibada, kuipenda na kuushughulisha mwili wake nayo.
Mam Sajjad (as) pia anaelezea hivi uzuri wa mwezi mtukufu wa Ramadhani katika dua ya 45 ya Sahifah Sajjadiyah: "Amani iwe juu yako, ewe nyakati tukufu zaidi na Ewe mwezi bora zaidi / Amani iwe juu yako, ewe rafiki ambaye uwepo wake ni wa thamani na kutokuwepo kwake ni kuchungu / Amani iwe juu yako, ewe Mfariji, ambaye kuja kwako huleta furaha."
Maneno haya yanaonyesha umuhimu wa shauku na mapenzi ya moyo kwa ajili ya kuelewa umuhimu wa funga ya mwezi wa Ramadhani na athari zake, katika kuzindua nyoyo na kutuhimiza tujishughulishe zaidi na faradhi hii muhimu ya Mwenyezi Mungu.
*******
Kiashiria kingine katika kunufaika na baraka za Ramadhani ni kuzingatia desturi za kufunga. Kuzingatia taratibu za ibada yoyote huongeza uzuri na ukamilifu wake. Kusoma Qur'ani, kuwasaidia masikini, kuzuia ulimi kutamka maovu na kuwafanyia wema wengine ni miongoni mwa adabu na desturi za saumu.
Katika dua zake za kuvutia, Imam Sajjad (a.) alimwomba Mwenyezi Mungu ampe uwezo wa kufanya ibada ipasavyo katika mwezi wa Ramadhani. Anasema: "Ewe Mungu wangu! Tujaze ibada yako katika mwezi wa Ramadhani / zipambe nyakati zake kwa utiifu wetu /tusaidie kufunga mchana na kuswali usiku."
Tunasoma hivi katika dua ya siku ya tano ya mwezi mtukufu wa Ramadhani: "Ewe Mwenyezi Mungu! Nijaalie katika siku hii niwe katika wenye kusamehewa, na nijaalie niwe katika waja wako wema, na nijaalie kuwa katika walii wako wa karibu, kwa haki ya huruma yako Ewe Mbora wa wenye kurehemu."
******
Katika dua ya siku ya tano ya mwezi huu mtukufu, kwanza tunatubu na kumwomba Mwenyezi Mungu atusamehe madhambi zetu. Imam Ali (as) anafafanua toba kama ifuatavyo: “Kuomba msamaha ni daraja ya juu kabisa na ina maana sita: Kujutia jambo, uamuzi wa kuacha dhambi, kupeana haki za watu, kufidia faradhi zilizopotea, kuharibu nyama haramu kwa huzuni, na kuonjesha mwili uchungu wa utiifu, kama ulivyouonjesha utamu wa dhambi." Kuhusu umuhimu wa kuomba toba na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tunarejea kwenye Sura ya Taha, Aya ya 82, ambayo inasema: “Na hakika Mimi ni Mwingi wa Kusamehe kwa anayetubia, akaamini na akatenda mema, tena akaongoka."
Tukiwa katika duru hii yenye nuru na baada ya kufaulu kuomba maghfira, tunamwomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake wema na watiifu. Watumishi waadilifu ni wale walio na uhusiano mkubwa na endelevu na Mwenyezi Mungu. Hadith iliyopokelewa kutoka kwa Mtume Mtukufu Muhammad al-Mustafa (saw) inasema kwamba Mwenyezi Mungu amesema: "Nimewatayarishia waja wangu wema malipo ambayo hakuna jicho lililoyaona wala sikio lililoyasikia."
*************
Tunamwomba Mwenyezi Mungu atuweke karibu na waja wake wema. Waja ambao kamwe hawaghafiliki kumkumbuka Mola wao na kumtii. Wanaomwabudu na kumtii si kwa sababu ya kuogopa Jahanamu wala kuwa na tamaa ya Pepo bali kwa ajili ya kupata radhi zake tu. Mwenyezi Mungu anasema kuhusu waja hawa wema: “Naapa kwa utukufu Wangu, ikiwa mja yeyote mwaminifu ataweka radhi yangu mbele ya matamanio yake, nitamfanya asiwe mhitaji na ashughulishwe tu na mambo ya Akhera. Nitazifanya mbingu na ardhi kuwa ni zenye kudhamini riziki yake, na mimi kuwa nyuma yake katika kila biashara (jambo) anayofanya.” (Hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw).
Wapendwa wasikilizaji na kufikia hapa ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki ambacho tumekuleteeni katika mfululizo wa vipindi vya Ramadhani, Dhifa ya Mwenyezi Mungu". Tunatumai kuwa kipindi cha leo kimekunufaisheni na kukuhimizeni mfanye juhudi za kutosha kwa ajili ya kufaidika na baraka chungu tnzima zilizoko kwenye mwezi huu mtukufu. Tufanyeni hima kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu kwa kuomba na kutumia vizuri fursa za mwezi huu.
Wassalaam Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh