Utafiti: Uislamu ndiyo dini inayokuwa kwa kasi zaidi duniani
(last modified Wed, 11 Jun 2025 07:53:24 GMT )
Jun 11, 2025 07:53 UTC
  • Utafiti: Uislamu ndiyo dini inayokuwa kwa kasi zaidi duniani

Utafiti mpya umebainisha kuwa, idadi ya Waislamu duniani imeongezeka zaidi kuliko dini nyingine zote kwa pamoja, katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Utafiti huo uliochapishwa na Kituo cha Utafiti cha Pew's Global Religious Landscape umeeleza kuwa, Waislamu ndio wafuasi wa kundi la kidini linalokuwa kwa kasi zaidi duniani, baada ya kutathmini mabadiliko ya idadi ya watu kwa mujibu wa dini zao duniani kati ya 2010 na 2020.

Utafiti huo umesema kuwa, wakati Ukristo ukisalia kuwa dini kubwa zaidi yenye waumini bilioni 2.3, sehemu yake ya idadi ya watu duniani imepungua kwa takriban asilimia 1.8 tangu mwaka 2010, huku sehemu ya Uislamu ikiongezeka. Umesema idadi ya Waislamu inaongezeka hasa kwa sababu ya ukuaji wa asili wa idadi ya watu, na kufanya Uislamu kuwa dini inayokuwa kwa kasi zaidi duniani.

Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa, idadi ya Waislamu duniani iliongezeka kwa milioni 347 katika kipindi cha miaka 10, na kubainisha kuwa mabadiliko ya idadi ya Waislamu "hayana uhusiano wowote na watu kuingia au kutoka katika dini hiyo" katika ngazi ya kimataifa.

"Tunaangalia sifa za idadi ya watu wa makundi haya, muundo wao wa umri, ni watoto wangapi wanaozaliwa, wana elimu kiasi gani, kwa sababu sifa hizi za kidemografia huathiri ukubwa wa siku zijazo wa makundi ya kidini," Conrad Hackett, mwanademografia mkuu katika Kituo cha Utafiti cha Pew, amesema.

"Waislamu wana watoto wengi na ni wachanga zaidi, kwa wastani, kuliko waumini wa dini nyingine yoyote kuu," utafiti huo ulisema. "Kulingana na takwimu za kipindi cha 2015-2020, tulikadiria mwanamke Mwislamu angekuwa na watoto 2.9, kwa wastani, katika maisha yake, ikilinganishwa na watoto 2.2 kwa mwanamke asiye Mwislamu," imeongeza ripoti ya utafiti huo.

Uislamu ni dini ya pili kwa ukubwa duniani, ikiwa na karibu watu bilioni mbili, au karibu robo ya idadi ya watu wote duniani.