Iran, ulimwengu wa Kiislamu waadhimisha kumbukizi ya kuzaliwa Imam Ali AS
Wananchi Waislamu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamejiunga na wenzao kote duniani kuadhimisha siku ya kukumbuka kuzaliwa Amirul Muumin Ali (AS) Imam wa Kwanza wa Waislamu wa Kishia ulimwenguni.
Ali bin Abi Twalib (AS) alizaliwa katika nyumba tukufu ya al Kaaba tarehe 13 Rajab na katika nyakati za utotoni alilelewa na kupata elimu na mafunzo kutoka kwa Mtume Mtukufu (SAW).
Aidha alikuwa mwanaume wa kwanza kuukubali Uislamu; na alikuwa msaidizi mkuu wa Mtume Mtukufu (SAW) katika marhala zote za tablighi na kueneza mafunzo ya dini ya Uislamu za Mtume wa Uislamu.
Katika Kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Kuzaliwa Imam wa Kwanza wa Waislamu wa Kishia Ulimwenguni imepewa jina la "Siku ya Baba."
Katika siku hii kwa kawaida wananchi waumini na wamchao Mwenyezi Mungu wa Iran ya Kiislamu huadhimisha siku hii ya mazazi ya Imam Ali (AS) kwa sherehe mbalimbali kwa kukusanyika katika maeneo matukufu, ambaye kwa hakika ni baba wa maimamu.
Mamilioni ya waumini wameshiriki katika shughuli hiyo katika miji mbalimbali na shughuli zote za umma zimefungwa leo kwa ajili ya kumuenzi na kumkumbuka Amirul Muuminin, Ali bin Abi Talib (AS).
Ali bin Abi Talib AS ambaye ndiye Imam wav kwanza katika mlolongo wa Maimamu 12 watoharifu, ni mume wa binti ya Mtume Fatma Zahra as na baba wa Maimamu wawili watoharifu Hassan na Hussein AS.
Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu na wapigania ukombozi wote duniani kwa mnasaba huu wa kukumbuka kuzaliwa Imam wa Kwanza wa Waislamu wa Kishia ulimwenguni Imam Ali (AS).